Habari

Imewekwa: Aug, 01 2023

MAWAKILI WA SERIKALI WAPONGEZWA KWA UTENDAJI KAZI.

News Images

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi Sarah Mwaipopo amefanya ziara ya kikazi kwenye Ofisi za Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) zilizopo kwenye Mkoa wa Ruvuma na Iringa kwa lengo la kukagua utendaji kazi wa Ofisi hizo.Katika ziara hiyo, alifanya vikao na Mawakili wa Serikali wa Manispaa, Halmashauri na Ofisi za Mkuu wa Mkoa, wanaotekeleza majukumu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Aidha, alitembelea Mahakama Kuu Kanda ya Songea na Iringa na kupata fursa ya kufanya majadiliano na Majaji Wafawidhi kuhusu mashauri yanayoendeshwa katika Kanda hizo za Makahama yanayosimamiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Katika ziara hiyo, Bi Mwaipopo akiongea kwa niaba ya Dkt. Boniface Luhende, Wakili Mkuu wa Serikali, amewapongeza Mawakili wa Serikali kwa ushirikiano na kazi nzuri wanayoifanya ya usimamizi wa mashauri yanayofunguliwa na au dhidi ya Serikali.Aidha, amesisitizia umuhimu wa Mawakili wa Serikali kusimamia mashauri kwa ufanisi na kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miongozo na Hati za Mamlaka za uendeshaji mashauri zinazotolewa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Amewataka Mawakili wa Serikali kutoa taarifa kwa wakati za mashauri yote yanayofunguliwa na Serikali au dhidi ya Serikali, kutoa ushirikiano kwenye Ofisi wakati wa uandaaji wa mashauri, ushahidi na mashahidi wao wakati wa uendeshaji mashauri mahakamani.

Bi. Mwaipopo amewakumbusha Mawakili kuhakikisha wanakuwa vinara wa kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza katika utendaji na utekelezaji wa miradi mbalimbali na kuzalisha kesi dhidi ya Serikali kwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anapeleka fedha nyingi kwenye mikoa na halmashauri mbali mbali nchini ili kufanikisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Pia, ameongeza kuwa ushiriki na ushirikishwaji wa Mawakili wa Serikali ni muhimu kwenye hatua zote za uaandaji na utekelezaji wa mikataba kwa lengo la kuzuia migogoro inayoweza kuigharimu Serikali kuendesha mashauri na kulipa fidia kwa kadri vyombo vya haki vitakavyoelekeza. Amewakumbusha Mawakili kuzingatia sheria, kanuni za taratibu wakati wa uaandaji na upekuzi wa mikataba na kuhakikisha wanashirikisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kikamilifu na kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi wakati wa Kikao cha Mawakili wa Serikali kilichofanyika Septemba mwaka 2022, kwa lengo la kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza kwa taasisi kutokufuata taratibu katika utekelezaji wa majukumu.

Katika hatua nyingine, Bi Mwaipopo aliwasisitizia Mawakili wa Serikali kufanya vikao vya mara kwa mara vya pamoja na OWMS za Mikoa kwa lengo la kutathmini utendaji kazi wa mashauri yanayofunguliwa mikoani, mafanikio na changamoto wanazozipitia katika utekelezaji wa majukumu ya uendeshaji mashauri.

Pia, alipata fursa ya kufanya mazungumzo na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Ephery Sedekia na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Ilvin Mugeta kwa kuwa OWMS inashirikiana na kufanya kazi kwa karibu na Mahakama hizo kwenye kazi za uendeshaji wa mashauri. Mazungumzo hayo pia yalihusisha mifumo ya usimamizi wa mashauri baina ya taasisi hizo ambayo inapaswa kusomana ili kuhakikisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati pamoja na ufanyaji wa tafiti wa mashauri ambayo yanafunguliwa kwa wingi kwa mfano mashauri ya ardhi, kwa lengo la kuishauri Serikali na taasisi zake.

Waheshimiwa Majaji Mugeta na Sedekia wamesema kuwa OWMS inawapa ushirikiano wa kutosha katika uendeshaji wa mashauri ya Serikali na taasisi zake, jambo ambalo limeiwezesha Serikali kupata mafanikio katika mashauri ambayo yanaendeshwa na kukamilika.

Halikadhalika katika ziara hiyo, Bi. Mwaipopo ameonana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Steven Mashauri na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Bashir Muhoja na kuhaidi kuendeleza ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ya utekelezaji wa majukumu.

Mawakili wa Serikali Wafawidhi, Mkoa wa Ruvuma na Iringa, Egidy Mkolwe na Ansila Makyao, wameishukuru OWMS kwa kuwapatia ushirikiano, magari na vitendea kazi ambavyo vinawawezesha kutekeleza majukumu ya kuendesha mashauri ya Serikali ndani ya Mikoa wanayofanyia kazi

Mwaipopo amewaahidi Mawakili wote wa Serikali kuwa OWMS kwa kushirikiana na mamlaka nyingine ndani ya Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha kwenye masuala ya uendeshaji mashauri na mengineyo yanayohusiana na kufanya ziara endelevu za utendaji kazi ili kuhakikisha kuwa sheria, taratibu na kanuni zinazingatiwa katika mnyororo wa utoaji haki.