Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

Kazi na Majukumu

Kwa mujibu wa Muundo wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ina viongozi wakuu wawili ambao ni Wakili Mkuu wa Serikali ambaye ni mkuu wa taasisi na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali ni Msaidizi Mkuu wa Wakili Mkuu wa Serikali na Afisa Masuhuli ambaye anawajibika kusimamia majukumu ya kila siku ya taasisi na ni mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wote waliopo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Yafuatayo ni majukumu ya Wakili Mkuu wa Serikali : -

i) Kuratibu, kusimamia na kuendesha mashauri yote ya Madai na Usuluhishi yanayofunguliwa na Serikali/Taasisi zake au dhidi ya Serikali/ Taasisi zake ndani na nje ya Nchi. Taasisi ni pamoja na Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mamlaka na Mashirika ya Umma na pia kuingilia kati (intervene) na kuendesha mashauri yanayozihusu taasisi binafsi ambapo Serikali ina maslahi au kugusa mali za Umma,

ii) Kuishauri Serikali kwenye mambo yote yanayohusu mashauri ya madai na usuluhishi kwa weledi;

iii) Kuandaa, kufungua na kuitetea Serikali na Taasisi zake katika Mahakama na Mabaraza ya ndani na nje ya Nchi zikiwemo Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu, Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na Mahakama na Mabaraza ya Nchi za Nje na Mabaraza ya kimataifa. 

iv) Kusimamia na kuratibu mwenendo wa mashauri yote ya Madai na usuluhishi yanayoihusu Serikali ambayo yapo Mahakamani na kwenye Mabaraza ya ndani na nje ya Tanzania ili kuhakikisha Serikali inapata uwakilishi stahiki, kwa ueledi mkubwa na wenye viwango;

v) Kusimamia na kutoa miongozo kwa maafisa sheria na Mawakili wa Serikali ambao wanahusika katika uendeshaji wa mashauri ya Madai yanayoihusu Serikali;

vi) Kusimamia na Kuratibu mashauri yote ya Madai na ya Usuluhishi yanayoihusu Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Idara mbalimbali na Mashirika ya Umma yaliyo katika Mahakama na Mabaraza;

vii) Kuingilia kati na kuchukua hatua stahiki kwenye mashauri ya Madai yote yaliyo katika Mahakama yoyote ambayo yana maslahi ya umma;

viii) Kutoa Maelekezo juu ya suala lolote kwa Afisa yeyote wa umma kwa ajili ya kuwezesha usimamizi mzuri wa Mashauri yote ya Madai;

ix) Kuhakiki na kupata idadi ya Mashauri yote ya Madai yanayoihusu Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma na kuzipatia ufumbuzi;

x) Kufanya tafiti Mbalimbali za Kisheria ili kuhakikisha Serikali inapata uwakilishi na utetezi wenye hadhi ya juu pale inapokuwa na Mashauri Mahakamani ndani na nje ya Nchi;

xi) Kutambua mashauri mbalimbali ya Madai yasiyo na tija na ambayo yanayoweza kuongeza hasara kwa Serikali na kuyatatua kwa njia za majadiliano na maridhiano nje ya Mahakama;

xii) Kufanya tathmini ya kina ili kubaini chanzo cha mashauri ya Madai yanayoihusu Serikali na namna ya kuyashughulikia kwa ufanisi;

xiii) Kuweka utaratibu mzuri utakaowezesha Wizara, Idara na Taasisi za Umma, kutunza na kutoa taarifa/kumbukumbu za Mashauri ya Madai yanayosimamiwa katika Wizara, Idara na Taasisi husika ya Umma;

xiv) Kufanya vikao mbalimbali na wadau juu ya mashauri yasiyo na tija kwa Serikali na kuangalia ni kwa jinsi gani yanaweza kumalizika nje ya Mahakama na hivyo kuipunguzia Serikali gharama; na

xv) Kuandaa Taarifa za Mashauri inayoendesha na kuiwasilisha kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Katiba na Sheria.