Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

Majukumu ya Idara

IDARA YA UTAWALA NA RASILIMALI WATU

Idara hii inahusika na usimamizi wa rasilimali watu na utawala. Idara hii ina sehemu mbili (2) ambazo ni:  

Sehemu ya Utawala

Sehemu hii inasimamia masuala yote yanayohusiana na uendeshaji wa ofisi.

Sehemu ya Usimamizi wa Rasilimali watu

Sehemu hii inasimamia masuala yote ya kiutumishi pamoja na usimamizi wa rasilimali watu.

IDARA YA MIPANGO

Idara hii inahusika na kutoa ushauri wa kitaalam kwenye masuala ya mipango, bajeti, ufuatiliaji na tathmini. Idara ina vitengo viwili, Kitengo cha Mipango na Bajeti (Planning and Budgeting); na Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini (Monitoring and Evaluation).

IDARA YA USIMAMIZI WA MASHAURI NA UDHIBITI UBORA

Idara hii ni inahusika na uratibu, usimamizi na udhibiti wa ubora wa huduma zinazotolewa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Idara hii imegawanyika katika sehemu kuu mbili (2) zinazoongozwa na Wakurugenzi Wasaidizi ambazo ni:

  1. Uratibu na Usimamizi wa Mashauri ya madai na usuluhishi;
  2. Udhibiti wa ubora.

Sehemu ya Uratibu na Usimamizi wa Mashauri ya Madai na Usuluhishi

Sehemu hii inahusika na uratibu na usimamizi wa mashauri ya madai na usuluhishi ndani nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa mashauri hayo yanaendeshwa kwa weledi.

Sehemu ya Udhibiti Ubora

Sehemu hii inasimamia na kuhakikisha kuwa utekelezaji wa majukumu yote ya ofisi unatekelezwa kwa ufanisi na ubora unaotakiwa.

IDARA YA MADAI

Idara ya Madai ni moja kati ya Idara ya kiutendaji inayotekeleza majukumu ya kuratibu, kusimamia na kuiwakilisha Serikali na Taasisi zake katika mashauri yote ya Madai ndani na nje ya nchi. 

Idara imegawanywa katika sehemu kuu tatu zinazoongozwa na Wakurugenzi wasaidizi, ambazo ni:

  1. Madai ya Ndani ya Nchi (Kitaifa);
  2. Madai ya nje ya Nchi (Kimataifa); na
  3. Madai ya Kikatiba, Haki za Binadamu na Uchaguzi.

Sehemu ya Madai ya Ndani ya Nchi (Kitaifa)

Sehemu hii inahusika na uratibu, usimamizi, na uendeshaji wa mashauri yote ya Madai Kitaifa yaliyofunguliwa dhidi ya au kwa niaba ya Serikali na Taasisi zake katika Mahakama na mabaraza ya ndani ya Nchi. Hali kadhalika, kuingilia kati na kuendesha mashauri ambayo Serikali ina maslahi  au kugusa mali za Umma.

Sehemu ya Madai ya Nje ya Nchi (Kimataifa)

Sehemu hii inahusika na kuratibu, kusimamia na kuendesha mashauri yote ya Madai kimataifa yaliyofunguliwa dhidi ya au kwa niaba ya Serikali na Taasisi zake katika Mahakama za nje ya nchi.

Sehemu ya Madai ya Kikatiba, Haki za Binadamu na Uchaguzi

Sehemu hii inahusika na kuratibu, kusimamia na kuendesha mashauri yote ya Kikatiba, Haki za Binadamu, maombi ya marejeo (Judicial Review) na Uchaguzi dhidi ya Serikali katika Mahakama zote. Aidha, sehemu hii inasimamia mashauri yote yanayofunguliwa kupinga vifungu vya sheria mbalimbali na masuala yanayohusu ukiukwaji wa Haki za binadamu na katiba. Pia, sehemu hii inasimamia mashauri yaliyofunguliwa dhidi ya Serikali katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

IDARA YA USULUHISHI

Idara ya Usuluhishi ni moja kati ya Idara ya kiutendaji inayotekeleza majukumu ya kuratibu, kusimamia na kuiwakilisha Serikali na Taasisi zake katika mashauri yote ya Usuluhishi ndani na nje ya nchi.  Idara ya Usuluhishi imegawanywa katika sehemu kuu mbili zinazoongozwa na Wakurugenzi Wasaidizi, ambazo ni:

  1. Usuluhishi wa ndani ya Nchi (Kitaifa);
  2. Usuluhishi nje ya nchi (Kimataifa)

Sehemu ya Usuluhishi wa Kitaifa

Sehemu hii inahusika na kuratibu, kusimamia na kuendesha mashauri yote ya Usuluhishi yaliyofunguliwa dhidi ya au kwa niaba ya Serikali na Taasisi zake katika Mabaraza ya Usuluhishi ndani ya nchi.  Hali kadhalika, kuingilia kati na kuendesha mashauri ya usuluhishi ambayo Serikali ina maslahi  au kugusa mali za Umma.

Sehemu ya Usuluhishi wa Kimataifa

Sehemu hii inahusika na kuratibu, kusimamia na kuendesha mashauri yote ya Usuluhishi yaliyofunguliwa dhidi ya au kwa niaba ya Serikali na Taasisi zake katika Mabaraza ya Usuluhishi ya nje ya nchi.