Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

SG AKAGUA UJENZI WA JENGO LA OFISI MTUMBA, DODOMA

Imewekwa: 31 January, 2026
SG AKAGUA UJENZI WA JENGO LA OFISI MTUMBA, DODOMA

Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi akagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali linaloendelea kujengwa kwenye mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma.

Ujenzi wa jengo hilo umefikia kiwango cha asilimia 73 na umegharimu jumla ya shilingi bilioni 16 na ili liweze kukamilika zitatumika jumla ya shilingi bilioni 26 na linajengwa kwa fedha za Serikali.

Dkt. Possi amemtaka mkandarasi, SUMA JKT na mshauri elekezi, TBA kuhakikisha kuwa jengo hilo linakamilika kwa kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa ili liweze kutumika kwa muda mrefu. Pia, amemwelekeza mkandarasi kuwa kisima cha maji ya ardhini kilichochimbwa kitunzwe ili maji yake yaweze kutumika wakati wa msimu wa kiangazi na matumizi mbali mbali ikiwemo utunzaji wa mazingira ili kuifanya Dodoma kuwa ya kijani.

“Nategemea kupata jengo lenye ubora na viwango vinavyotakiwa ili liweze kutumika kwa muda mrefu kwa lengo la kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza tija na ufanisi katika mnyororo wa utoaji haki nchini,” amesisitiza Dkt. Possi.

Pia, ameongeza kuwa tunahitaji jengo liishe mapema mwaka huu ili tuhamie Dodoma kwa kuwa Ofisi hii inafanya kazi kwa karibu na Mahakama ya Tanzania ambayo tayari imehamia Dodoma.

Dkt. Possi aliambatana na Menejimeneti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, mwakilishi wa mkandarasi, Meneja Ujenzi Kanda ya Mashariki wa SUMA JKT, Kanali Saul Chiwanga na mwakilishi wa mshauri elekezi, Kaimu Meneja Miradi wa TBA, ndugu Daniel Nkruma.