DKT. POSSI: VIONGOZI NI TASWIRA YA TAASISI NA SERIKALI KWA JAMII
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeendesha mafunzo kwa viongozi wa taasisi hiyo na menejimenti yake ambayo yamefanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki ambapo pamoja na mafunzo hayo viongozi hao wamejitathmini utendaji kazi wao wa kila siku, wamepatiwa mafunzo ya uongozi ikiwemo usimamizi na mgawanyo wa majukumu, usimamizi wa muda, itifaki na ustaarabu.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi alifungua mafunzo hayo na kuwaeleza wajumbe wa menejimenti ya Ofisi hiyo kuwa viongozi ni taswira ya taasisi na Serikali kwa ujumla ambapo amewaeleza kuwa kiongozi yeyote awe Mkuu wa Idara au Mkuu wa Kitengo atambue kuwa anabeba taswira ya taasisi anayofanyia kazi na Serikali kwa ujumla popote alipo, iwe kazi au unapoishi, hivyo ni muhimu kuzingatia sheria, taratibu, kanuni, maadili ya uongozi, mila na desturi za uongozi.
“Kila mmoja ajitambue wadhifa alionao na bendera anayopeperusha kwa niaba ya Serikali na kwa wale tunaowaongoza. Tuwe walezi kwa kuzingatia kuwa muda mwingi tupo mahali pa kazi kuliko familia zetu, watu tunaofanya nao kazi wafurahie kufanya kazi na wewe badala ya kukasirika, tujitathmini na kutafakari utendaji kazi wetu ili kuwa na matokeo mazuri mahali pa kazi na kujipa muda wa kujisahihisha huku tukifanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni, tuwe wabunifu na tufanye ufuatiliaji wa majukumu,” amesisitiza Dkt. Possi.
Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo amesema kuwa kikao hicho cha faragha na mafunzo hayo ni muhimu kwa wajumbe wa menejimenti wa Ofisi hiyo ili kupata muda wa kutathmini utendaji kazi na ana amini kuwa mafunzo hayo yataleta mabadiliko katika taasisi, kuwawezesha kuwafahamu na kuwasimamia vizuri wasaidizi wao, kumiliki kazi zao, kufanya maamuzi kwa wakati na kuzingatia muda katika utekelezaji wa majukumu.
Akitoa mada kuhusu uongozi na mgawanyo wa majukumu kwa wajumbe hao, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, ndugu Kadari Singo, amewapongeza viongozi wa Ofisi hiyo kwa kuandaa na kushiriki mafunzo hayo na ametoa rai kwao kujenga utaratibu wa kuwajenga wasaidizi wao ili wanapoondoka kwenye nafasi zao wawe na watu wa kuhakikisha mifumo inafanya kazi.
Aidha, Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, ndugu Godwin Gonde Amani, aliwafundisha wajumbe wa menejimenti hiyo mada kuhusu itifaki na ustaarabu ambayo ilijikita kwenye masuala ya muonekano wa mtu, mavazi, mawasiliano, tabia, mienendo, matumizi ya akili ya kuzaliwa, kuheshimu mamlaka na madaraka ya kiongozi, kutambua, kujali na kuthamini uwepo wa kiongozi.
“Iitifaki ni jambo muhimu Serikalini na katika uongozi kwa kuwa ni jambo nyeti lina athari chanya na hasi baina yako binafsi na mtu mwingine katika muonekano wa mavazi, salamu, mazungumzo na mawasiliano,” amesisitiza Mhadhiri Amani.
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imekuwa na utaratibu wa kuendesha mafunzo kwa viongozi wa Ofisi hiyo, kufanya kikao cha faragha kwa ajili ya kutathmini utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu mara moja kwa mwaka.