WAKILI MKUU SPORTS CLUB, RAS GEITA WATOSHANA NGUVU
Timu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imetoka sare ya bao 1-1 dhidi ya timu ya RAS Geita katika mchezo wa mashindano ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali (SHIMIWI) uliochezwa mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa tangu mwanzo, ulianza kwa kasi huku kila timu ikionekana kuwa na dhamira ya kupata bao la mapema. Hata hivyo, timu ya Wakili Mkuu iliyokuwa ya kwanza kuvunja ukuta wa RAS Geita baada ya kiungo wake, Egidy Mkolwe, kufunga bao dakika ya 15 ya kipindi cha kwanza.
Bao hilo liliipa nguvu zaidi timu ya Wakili Mkuu ambayo iliendelea kumiliki mchezo na kufanya mashambulizi kuelekea lango la RAS Geita ambapo safu yake ya ulinzi ikifanya kazi ya kuhakikisha inazuia mashambulizi ya wapinzani wao.
Juhudi za timu ya RAS Geita za kutafuta bao la kusawazisha hazikuzaa matunda katika kipindi cha kwanza ambapo hadi mwamuzi alipopuliza filimbi ya kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza, timu ya Wakili Mkuu ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi na timu zote ziliongeza mashambulizi katika kutafuta mabao. Wakili Mkuu Sports club walijaribu kuongeza bao la pili ili kujiwekea nafasi nzuri ya kushinda mchezo, wakati RAS Geita wakisaka bao la kusawazisha.
Baada ya kushambuliana kwa muda, RAS Geita walifanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 25 ya kipindi cha pili na kuufanya mchezo kuwa wa bao 1-1.
Baada ya bao hilo, timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu huku kila upande ukitafuta bao la ushindi. Hata hivyo, juhudi hizo hazikuzaa matunda hadi mchezo ulipomalizika.
Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika kocha wa timu ya Wakili Mkuu Sports club, ndugu Denis Lipiki alisema kuwa mchezo ulikuwa mzuri kwa kuwa timu yake ilianza mchezo huo kwa nguvu na kufanikiwa kupata bao la mapema.
Akizungumzia matokeo ya sare, ndugu Lipiki alisema kuwa kukosa umakini kwa wachezaji wake kulisababisha kufanya makosa ambayo yalisababisha timu pinzani kupata bao la kusawazisha dakika za mwisho za mchezo.
Katika michezo iliyochezwa awali kwenye uwanja wa Magereza kati ya timu ya Wakili Mkuu na RAS Morogoro, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana, wakati mchezo wat imu ya Wakili Mkuu Sports club na RAS Pwani zilitoshana nguvu kwa kutoka sare ya goli 1-1.
Kwa matokeo hayo, timu ya Wakili Mkuu Sports club imefanikiwa kujikusanyia jumla ya alama 6 na kuifanya timu hiyo kuwa miongoni wa timu ambazo hazijapoteza mchezo mpaka sasa.