Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

Wakili Mkuu Sports Club yaiduwaza Osha Sports Club

Imewekwa: 08 September, 2025
Wakili Mkuu Sports Club yaiduwaza Osha Sports Club

Timu ya Mpira wa Miguu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (Wakili Mkuu Sports Club), imefanikiwa kuiduwaza timu ya mpira wa miguu ya Wakala wa Serikali Mahala pa Kazi (OSHA) baada ya kibuka na ushindi wa bao 1-0 Katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa shule ya Msingi Mabatini jijini Mwanza.

Katika mchezo huo ulianza majira ya saa 4.00 asubuhi, timu ya Wakili Mkuu wa Serikali iliuanza mchezo huo kwa kasi hali iliyopelekea kufanya mashambulizi mengi ya hatari langoni mwa timu ya OSHA.

Timu ya mpira wa miguu ya Wakili Mkuu Sports Club, walisubiri mpaka dakika ya 17 ya kipindi cha kwanza baada ya mpira mrefu uliopigwa na mlinda mlango machachali ndugu Ditrick Lwambano na kumkuta kiungo hatari wa timu ya Wakili Mkuu wa Serikali ndugu Joseph Bundala aliyetuliza mpira huo kwa ustadi wa hali ya juu na kutoa pasi maridhawa kwa ndugu Egidy Mkolwe ambaye hakufanya ajizi na kuukwamisha mpira huo wavuni.

Kupatikana kwa bao hilo kuliamsha furaha, nderemo,hoi hoi na vifijo kwa mashabiki wa timu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambao waliendelea kuimba nyimbo mbalimbali zenye lengo la kuhanikiza ushindi wa timu yao mpaka timu hizo zilipoenda mapumziko ya kipindi cha kwanza cha mchezo huo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikiwa mbele kwa goli 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, iliendelea kulisakama lango la mpinzani wake bila huruma wakati wote wa mchezo kwa kupiga mashuti mengi langoni ambayo mengi yalitoka nje ya uwanja.

Baada ya kufanya mashambulizi mengi bila mafanikio nusura timu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali iandike bao la pili kufuatia shuti kali lililopigwa na mshambuliaji hatari wa timu hiyo ndugu Habibu Rajabu lililogonga mwamba na kutoka nje.

Akizungumza baada ya mchezo huo kocha wa timu ya Wakili Mkuu wa Serikali, ndugu Denis Lipiki amewapongeza wachezaji wake kwa kupata ushindi huo ambao umesaidia kuongeza ari ya kufanya vizuri kwenye michezo ijayo.

Ameongeza kuwa ushindi uliopatikana leo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na moyo wa kujitolea wa wachezaji hao pamoja na kufuata maelekezo ambayo amekuwa akiwapa yaliyopelekea wachezaji wake kucheza kama timu na kuelewana vyema wakati wote wa mchezo na kufanikiwa kupata ushindi huo.

Kwa upande wake nahodha wa timu hiyo, ambaye ndiye mfungaji wa bao pekee liloipatia ushindi timu ya Wakili Mkili Mkuu wa Serikali, Ndugu Mkolwe amewapongeza wachezaji kwa ushindi wa leo huku akitoa rai kwa timu pinzani kujiandaa kupokea pumzi ya moto katika mechi zinazofuata.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kuushukuru uongozi na Menejimenti ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano wanaoipa timu yake ikiwa ni pamoja na kusaidia kupata kambi nzuri, mwalimu mwenye weledi wa hali ya juu ambaye amekuwa chachu ya timu hiyo kufanya vizuri.

Aidha, timu ya Kamba ya Wanawake wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeendelea kufanya vizuri baada ya kuwavuta timu ya Kamba ya Wanawake wa Wizara ya Viwanda, bila huruma hatua ambayo imeongeza morali ya timu hiyo kuendelea kufanya vizuri katika michezo inayofuata.

Timu ya mpira wa miguu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imepangwa kundi E lenye timu za Mahakama ya Tanzania, Wizara ya Kilimo, OSHA na Wizara ya Madini, imeingia mawindoni leo kujiwinda na mchezo unaofuata dhidi ya timu ya Mahakama ya Tanzania, katika mchezo unaotarajiwa kupigwa kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Bwiru iliyopo Jijini Mwanza.