Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

TIMU YA KAMBA YA WANAWAKE WA OWMS YAIBUKA NA ALAMA MOJA MZUNGUKO WA KWANZA SHIMIWI

Imewekwa: 08 September, 2025
TIMU YA KAMBA YA WANAWAKE WA OWMS YAIBUKA NA ALAMA MOJA MZUNGUKO WA KWANZA SHIMIWI

Timu ya wanawake wa Ofisi ya Wakili Mkuu Wa Serikali, imefanikiwa kuibuka mshindi baada ya kupata alama moja kati ya alama mbili zinazotakiwa katika mzunguko wa kwanza wa mchezo wa kuvuta kamba wakati wa mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inayoendelea jijini mwanza.

Michuano hiyo iliyoanza leo tarehe 1 Septemba 2025 katika viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza, Timu ya kuvuta kamba ya Wanawake wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ilipata ushindi huo kwa kuwavuta Timu ya Wanawake wa Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, ikiwa ni mchezo wa kwanza wa kundi H uliozikutanisha timu hizo.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo Nahodha wa timu hiyo Bi. Magreth Lihawala amesema kuwa mafanikio hayo yaliyopatikana yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na maandalizi mazuri yaliyofanywa na timu hiyo ikiwa ni pamoja na kuzingatia maelekezo na mbinu za Mwalimu ndugu Denis Lipiki muda wote wa mazoezi.

Bi. Lihawala ameeleza kuwa, licha ya ugumu na uzoefu wa timu waliyocheza nayo, amewapongeza wachezaji wake kwa moyo wa kujituma na kupambana, wakati wote wa mchezo huo hasa katika mzunguko wa kwanza ambapo ndipo walipofanikiwa kupata ushindi huo kwa kuwavuta timu ya wanawake kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.

 Aidha, Nahodha wa timu Bi.Lihawala ameeleza kuwa, mpango uliopo katika michezo inayofata ni kuongeza umakini, jitihada na kufuata maelekezo ya mwalimu ili kuhakikisha wanashinda michezo ya mizunguko yote miwili hatua itakayosaidia timu hiyo kusonga mbele na kuibuka kidedea mwisho wa mashindano hayo.

Kwa upande wa timu ya Kamba ya Wanaume wa Ofisi ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wametoka suluhu mchezo wa mzunguko wa kwanza na kupoteza katika mzunguko wa pili wa mchezo huo huku timu ya mpira wa miguu wanaume wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikikubali kipigo cha goli moja bila majibu dhidi ya timu ya Wizara ya Kilimo.

Michuano ya SHIMIWI iiyoanza leo inategemewa kuhitimishwa tarehe 16 Septemba 2025 huku zaidi ya timu 70 zikitarajiwa kushiriki michezo mbalimbali ambayo ni mpira wa miguu, kuvuta kamba, Mpira wa pete, karata, bao, drafti na riadha.