WIZARA NA TAASISI KUPANGA PAMOJA MAENDELEO YA SEKTA YA SHERIA
Wizara ya Katiba na Sheria iko tayari kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na taasisi zilizo chini ya Wizara kupanga pamoja maendeleo ya Sekta ya Sheria nchini.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Dkt. Franklin Rwezimula wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka 2026 wa watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali unaofanyika jijini Arusha na unaoongozwa na kaulimbiu isemayo, “Utumishi wenye thamani kuelekea Dira 2050.”
Dkt. Rwezimula alisema kuwa Wizara hiyo iko tayari kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na taasisi zote zilizo chini ya Wizara hiyo katika kupanga pamoja maendeleo ya Sekta ya Sheria.
“Dkt. John Jingu, Katibu Mkuu wa Wizara atakutana na viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara na atatembelea taasisi zote ili kuwa na vikao vya pamoja na tuainishe mahitaji ya taaluma za taasisi zote ili kuwajengea uwezo watumishi hao waweze kufanya kazi kwenye taasisi yeyote iliyo chini ya Wizara hii kwa manufaa ya Serikali kwa ujumla,” amesema Dkt. Rwezimula.
Pia, alisema kuwa kupitia mkutano huu watumishi wataongezewa uwezo na weledi kwa kupatiwa mafunzo mbalimbali yanayolenga ustawi wa watumishi na kuwa na majadiliano yanayohusu Ofisi ili kujenga utu na umoja katika kutekeleza majukumu yao.
Dkt. Ally Possi, Wakili Mkuu wa Serikali amesema kuwa Wizara iangalie namna ya kuwekeza kwa wafanyakazi kuhusu masuala ya usimamizi wa mikataba kwa kuwa ni jukumu la Mawakili kuzuia migogoro.
“Hivyo, Wizara iangalie utaratibu wa kuhakikisha kuwa Wizara na taasisi za Serikali zinahakikisha Mawakili wa Serikali wanahusishwa kwenye maandalizi, majadiliano na utekelezaji wa mikataba ya uwekezaji na miradi mikubwa ya Serikali ili kupunguza migogoro na kulinda maslahi ya taifa,” alisisitiza Dkt. Possi.
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice E. Mtulo amesema kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ina utaratibu wa kufanya mkutano wa watumishi wote kila mwaka ili kuwapatia watumishi mafunzo mbalimbali ambayo yanalenga kujenga utumishi bora na wa kisasa. Bi. Mtulo amesema kuwa kutakuwa na mada mbalimbali ambazo zitatolewa na wakufunzi na wabobezi na zitahusu maadili na itifaki za Serikali: kuishi na kuonekana kitaaluma; utumishi wenye thamani na maadili ya utumishi wa umma; mawasiliano yenye ushawishi, ufanisi na ujenzi wa mahusiano kazini; akili hisia na nguvu ya kujitambua na kudhibiti hisia; elimu ya namna ya kusimamia afya; elimu ya uwekezaji, misingi ya uwekezaji, maandalizi ya kustaafu na kuishi vizuri baada ya kustaafu; na usimamizi wa fedha.
Mkutano huo unafanyika kwa siku mbili tarehe 21 na 22 Mei, 2026 na umehudhuriwa na watumishi wote wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutoka mikoa 18 ambayo ni Dar es Saalam, Morogoro, Dodoma, Shinyanga, Mwanza, Mara, Kagera, Tabora, Mtwara, Ruvuma, Mbeya, Iringa, Rukwa, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Kigoma.