Habari

Imewekwa: Apr, 28 2022

Waziri Pinda awataka Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kufahamu wajibu wao Mahala pa Kazi.

News Images

NAIBU Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Geofrey Mizengo Pinda (Mb), amesema ni wajibu wa kila mtumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, kuhakikisha anafahamu wajibu wake mahali pa kazi, ili aweze kutekeleza malengo aliyopangiwa na kuhakikisha anayakamilisha katika muda uliopangwa hatua itakayosaidia ofisi hiyo kufikia malengo yake kwa wakati.

Ameyasema hayo, wakati akifungua Kikao cha pili cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa mwaka wa Fedha 2021/22 kilichofanyika leo Aprili 8,2022 Jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa kuwa ni wajibu wa kila mtumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuhakikisha anafahamu wajibu wake mahali pa kazi, ili aweze kutekeleza malengo aliyopangiwa na kuhakikisha anayakamilisha katika muda uliopangwa ikiwa ni pamoja na kutunza vitendea kazi vya ofisi pamoja na kuwahi kazini.

Akizungumzia bajeti ya OWMS, Kiongozi huyo amesema anaamini Ofisi hiyo itakuwa imeandaa bajeti yake kwa kufuata utaratibu wa Medium Term Expenditure Framework (MTEF), Kwa kuwa huu ndio utaratibu ambao bajeti huandaliwa kulingana na mipango iliyoainishwa kwenye Mpango kazi wa taasisi husika kwa kuzingatia vyanzo vya mapato na rasilimali zilizopo, kwa sababu Mtindo huu wa bajeti huonesha wazi utendaji wa kila idara hususani kwa mtu mmoja mmoja kulingana na vipimo vya utendaji kazi wake.

“Nichukue nafasi hii kuwataka wafanyakazi wa OWMS kufuata utaratibu unaoelekezwa na Bajeti husika. Mtakapokuwa mnafanya mapitio ya Bajeti ya nusu mwaka hapo baadaye, mtaona ni nani au Idara gani haikufanya kazi kulingana na malengo ya OWMS na hivyo kupata nafasi ya kurekebisha mapungufu mtakayoyabaini,” amesema Mhe. Pinda.

Aidha Mhe. Pinda amewahakikishia wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Wizara kuwa wataendelea kuiunga mkono ofisi hiyo kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya huku wakiendelea kufanyia kazi changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili ili waweze kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Kuhusu namna atakavyoshughulikia Changamoto zingine kiongozi huyo aliahidi kuzichukua na tutazishughulikia kwa kushirikiana na viongozi wengine wa Serikali ikiwa ni pamoja na kuziwasilisha zile changamoto za kiutumishi kwa Wizara husika ili ziweze kushughulikiwa kwa mujibu wa kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.

Akitoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Pinda aliwataka wajumbe hao kulitumia Baraza la Wafanyakazi kuhimiza kila mtumishi kujua wajibu wake wa kutumia muda wa kazi ipasavyo kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuiwezesha OWMS kusonga mbele katika kutekeleza maagizo ya serikali pamoja na kutoa huduma sitahiki kwa wakati.

Awali, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniface Nalija Luhende, ambaye pia ni Mkamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, amesema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali iliongezewa bajeti yake kutoka Shilingi Bilioni 11.48 kwa Mwaka wa Fedha 2020/21 hadi Bilioni 12.13 kwa Mwaka wa Fedha 2021/22 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 5.4.

Kiongozi huyo amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassani kwa kuona umuhimu wa ofisi yake uliopelekea kuongezeka kwa bajeti hatua ambayo itasaidia ofisi yetu kutekeleza majukumu yetu kwa ufasaha pamoja na kupunguza changamoto za ufinyu wa bajeti zilizokuwepo awali.

Kuhusu mashauri yaliyoendeshwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema kuwa ofisi hiyo imefanikiwa kuendesha mashauri ya madai 1,102 na ya Usuluhishi 117 na hivyo kufanya jumla ya mashauri yaliyoendeshwa kwa kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa 1,219.

Dkt. Luhende ameongeza kuwa jumla ya mashauri 450 yalimalizika ampapo Mashauri ya Madai yaliyomalizika na Serikali kushinda ni 444 huku Mashauri ya Usuluhishi yakiwa 6 na kupelekea Serikali kuokoa kiasi cha Shilingi Bilioni 236.6, ambazo kama serikali ingeshindwa basi Kiasi hicho cha fedha kingelipwa kwa walalamikaji waliofungua mashauri hayo katika Mahakamani mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Aidha, akizungumzia eneo la rasilimali watu, Makamu Mwenyekiti wa Baraza hilo amesema kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imeweza kujaza nafasi mbalimbali za ajira ambazo zimesaidia kujaza nafasi zilizokuwa wazi kwa lengo la saidia kuongeza nguvu katika maeneo ndani ya ofisi hiyo.

“tumefanikiwa kupata vibali vya kuajiri watumishi 23 wapya, watumishi 3 kwa nafasi ya ajira mbadala na mtumishi 1 wa kuhamia. aidha Ofisi imeweza kujaza nafasi hizo na kufikia jumla ya watumishi 159,” amesema Dkt. Luhende.