Habari

Imewekwa: Dec, 29 2021

Watumishi 60 wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wapandishwa Madaraja

News Images

Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alilolitoa Mei Mosi Mwaka huu kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi la kutaka watumishi wote wenye sifa wapandishwe madaraja, limeanza kutekelezwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambapo tayari watumishi 60 wameshapandishwa madaraja yao.

Mkurugenzi wa Raslimali watu katika Ofisi hiyo, James Kibamba aliyasema hayo ofsini kwake alipokuwa anazungumzia zoezi hilo ambapo amesema limefanyika na kukamilika kwa ufanisi.

“Watumishi 59 walioonekana kuwa na sifa walipandishwa madaraja baada ya uchambuzi na uhakiki kukamilika na mtumishi mmoja alibadilishiwa kada na hivyo kufanya idadi kamili kuwa watumishi 60 waliopanda madaraja,” alisema Kibamba.

Alisema watumishi hao waliopandishwa madaraja na aliyebadilishiwa kada walipitishwa katika mifumo ya kiutumishi na wataanza kupata mishahara ya vyeo vyao vipya.

Kibamba alisema kuwapandisha watumishi madaraja katika Ofisi kunasaidia kuongeza ufanisi wa kazi kwa kuwapatia motisha watumishi wengine pamoja na kuwawezesha baadhi ya mawakili kuhudhuria Mahakama za juu.

Hata hivyo Kibamba amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na ufanisi ili kufikia malengo ya Taasisi hiyo pamoja na Serikali kwa ujumla.

Ofisa Tawala Mwandamizi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Geofrey Annaniah alisema tayari Ofisi hiyo imepata kibali cha kuajiri makatibu muhtasi 15 na madereva wanane kwa ajili ya kujaza nafasi zilizoachwa wazi kwa lengo la kuongeza ufanisi katika ofisi za mikoa.

Alisema Ofisi hiyo imeendelea kujaza nafasi za watumishi kutoka watumishi wawili wakati Ofisi hiyo inaanzishwa mwezi Februali 2018 hadi kufikia watumishi 144 mwezi juni 2021.

Alisema lengo la Ofisi hiyo ni kuongeza watumishi kufikia 312 idadi ambayo ndiyo inayokubalika kwa mujibu wa ikama ya Ofisi hiyo ya Wakili Mkuu wa Serikali.

“Tayari Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeahidi kutupatia watumishi wengine katika mwaka huu wa fedha wa 2021/2022,” alisema Annaniah.

Hata hivyo alisema ofisi hiyo imeshafanikiwa kuweka mawakili wanaoiwakilisha Serikali katika mashauri ya madai na usuluhishi katika mikoa 15 nchini ili kuongeza ufanisi wa kazi.

Aliitaja mikoa ambayo tayari mawakili wa Serikali wameshawekwa kuwa ni Dodoma, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Mara, Mbeya Iringa, Ruvuma, Arusha, Tanga, Kilimanjaro, Tabora, Kigoma, Rukwa na Mtwara.

Alisema lengo la Ofisi hiyo ni kuwa na wawakilishi katika mikoa yote nchini na kwamba mpaka sasa harakati zinaendelea za kuajiri wengine kwa ajili ya mikoa ambayo bado haina wawakilishi hao.

Naye Ofisa Utumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Neema Baltazary alisema ofisi hiyo imeandaa mpango wa mafunzo ya muda mrefu nay a muda mfupi kwa watumishi ili kukuza ujuzi na kuboresha utendaji.

Alisema mpango huo wa mafunzo utawahusisha watumishi kutoka idara na vitengo vyote vya ofisi hiyo ili kujiendeleza katika kada zao na kwamba watakaoshiriki mafunzo hayo watatunukiwa vyeti vya ngazi mbalimbali.