Habari

Imewekwa: Nov, 15 2019

Tumiemi mifumo ya Tehama kutatua changamoto zilizopo

News Images

Watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wametakiwa kuzingatia matumizi bora ya Tehama ili waweze kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo hatua itakayosaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Bw. James Kibamba wakati akifungua mafunzo ya Tehama kwa niaba ya Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Gabriel Malata yaliyofanyika leo ndani ya ukumbi wa mikutano wa ofisi hiyo uliopo jijini Dar es Salaam.

Akielezea namna watakavyonufaika na mafuzo hayo, Mkurugenzi huyo amesema mfumo huo utasaidia kuwarahisishia watumishi hao upatikanaji wa majalada kwa wakati, tofauti na awali ambapo mtumishi angepaswa kusubiri kwa siku mbili au tatu kulipata faili hilo.

Bwa. Kibamba amewaasa watumishi hao kutoiogopa mifumo hiyo kwa kuwa mifumo hiyo ni sawa na majalada yaliyokuwa yanatumika hapo awali huku akiwaomba kujenga tabia ya kutumia mifumo hiyo mara kwa mara hasa mfumo wa barua pepe.

Akizungumzia changamoto za mifumo hiyo Mkurugenzi huyo amesema nivyema watumishi hao wakaainisha changamoto zote wanazokutana nazo na kuziwasilisha kwa wataalamu wa Tehama ili ziweze kufanyiwa kazi kwa manufaa ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Akizungumzia faida za mfumo huo Afisa Kumbukumbu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Athumani Zunda amesema kuwa kupitia mfumo huo sasa watumishi hao hawatalazimika kuwa na mafaili mengi mezani badala yake watapaswakufanyia kazi kwenye mfumo hatua itakayopunguza kuwa na nyaraka nyingi mezani bila sababu.

Alisistiza kuwa kwa kutumia mfumo huo mtumishi ataweza kupakia nyaraka tafautitofauti kwenye faili moja tofauti na ilivyokuwa awali ambapo watumishi walilazimika kutenganisha nyaraka hizo jambo lililosababisha mtumishi mmoja kuwa na mafaili mengi pasipo na ulazima wowote.

Bw. Zunda alieleza kuwa uwepo wa mfumo huo sasa umerahisisha utendaji kazi kwani sasa mafaili yanaweza kutembea kiurahisi na kumfikia mlengwa kwa wakati ukilinganisha na mwazo ampapo walitumia muda mwingi kujua lilipo faili husika ili waweze kulifanyia kazi.

Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Tehama Bw. Aziz Makaburi amewasihi watumishi hao kuitumia vyema mifumo hiyo huku akiwahakikishia kuwa mifumo hiyo itawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi tofauti na ilivyokuwa huko nyuma.

Amesema kuwa mifumo hiyo ni salama zaidi kwa kuzingatia ukweli kuwa sio rahisi kwa mafaili kupotea kwa kuwa faili likishaingizwa katika mfumo ni vigumu sana kuliondoa tofauti na ilivyokuwa zamani ampapo mtu angeweza kuliondoa kirahisi hivyo kupelekea upotevu wa nyaraka za ofisi kirahisi.

Bwa. Makaburi ameongeza kuwa matumizi wa mifumo yatawasaidia kutunza nyaraka zao kielektroniki hivyo italeta tija katika kuhakikisha mafaili hayo yanapatikana kirahisi pale yatakapohitajika hatua itakayosaidia kuweza kufanyiwa kazi kwa urahisi na ndani ya muda uliopangwa.

Mfumo wa masjala mtandao ni moja kati ya mifumo mitano inatotumiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kuhakikisha inakwenda na wakati katika matumizi ya Sayansi na Tekinolojia, mifumo mingine inayotumiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ni pamoja na mfumo wa vibali serikalini, mfumo wa barua pepe, mfumo wa uendeshaji wa mashauri na Mfumo shirikishi wa kusimamia utendaji kazi na rasilimali za Taasisi.