Habari

Imewekwa: Nov, 15 2021

Serikali Mbioni Kuanzisha Mfumo wa Kupima Utendaji Kazi kwa Mawakili

News Images

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, amesema kuwa serikali ina mpango wa kuanzisha mfumo wa kupima utendaji wa Mawakili wake ili kuhakikisha wanafikia malengo waliyojiwekea.

Dkt. Feleshi amezungumza hayo mapema leo wakati alipotembelea Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa lengo la kujitambulisha kwa Menejimenti Pamoja na watumishi wa ofisi hiyo ili kujionea namna wanavyotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Amesema kuwa mfumo huo wa kupima utendaji kazi kwa watumishi utaisaidia Serikali na Ofisi ya Wakli Mkuu Serikali kwa ujumla kujua utendaji kazi wa mtumishi mmoja moja hatua itakayosaidia kuongeza kasi ya uendeshaji wa mashauri yanayoihusu Serikali na Taasisi zake.

“Mipango yetu ni kuwa na Taasisi Bora ya kisheria katika kusimamia, kuratibu na kuendesha mashauri yote ya Madai na Usuluhishi yayoihusu Serikali”, alisema Dkt. Feleshi.

Kupitia mfumo huo Serikali itapata nafasi nzuri ya kujua idadi na aina ya mashauri yanayoendeshwa na Wakili mmoja mmoja hivyo itasaidia kurahisisha ufuatiliaji wa mashauri kwa ukaribu ili kuharakisha uendeshaji wa mashauri hayo na kuhakikisha yanamalizika kwa wakati.

Aidha, amewataka Mawakili Waandamizi kuhakikisha wanawasimamia na kuwajengea uwezo Mawakili wengine kwa lengo la kuhakikisha wanapata uzoefu wa kutosha ili waweze kusimamia vyema mashauri yote yanayoihisu serikali.

Dkt Feleshi amewasisitiza viongozi hao kuwa ni muhimu kwao kuendelea kuainisha changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika kusimamia na kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwani kwa kufanya hivyo itaisaidia serikali kupiga hatua Zaidi kutika uendeshaji wa mashauri yake kwa ufanisi Zaidi.

Kiongozi huyo amewasihi watumishi wa ofisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa juhudi amani na mshikamano huku akiahidi kuchukua changamoto zinazowakabili na kwenda kuzifanyia kazi kwa lengo la kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi kwa kila tumshi na ofisi kwa ujumla.

Dkt. Boniface Luhende amemshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kufanya ziara ofisini hapo na kusema kuwa Ofisi imejifunza mengi na itakwenda kufanyia kazi ushauri uliotolewa na kiongozi huyo ikiwepo kuweka mfumo mzuri wa kupima utendaji kazi wa watumishi wa ofisi hii.

“Ofisi imeshaanza maboresho na sasa tunajaribu kuweka mfumo wa kujua viwango vya utendaji kazi kujua watumishi wangapi wapo ofisi na wangapi hawapo na wanafanya nini ingawa bado hatujafika huko”. Dkt Luhende

Hii ni ziara ya kwanza kwa kiongozi huyo tangu kuteuliwa kushika wadhifa huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 12 septemba 2021.