Habari

Imewekwa: Aug, 09 2023

Rais Samia: Ongezeni Tija na Ubunifu katika Shughuli za Kilimo.

News Images

Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa Wakulima Nchini Kuongeza Tija na ubunifu katika Shughuli za Kilimo ambapo amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira Bora na wezeshi ili kuhakikisha Kilimo kinawakwamua wakulima kimaisha nchi nzima.

Rais Samia amesema hayo leo tarehe 08.08.2023 wakati akihitimisha sherehe za Kilele Cha Maonesho ya kimataifa ya Kilimo Nanenane yaliyofanyika Uwanja John Mwakangale Mkoani Mbeya.

Akizungumza na wananchi walioshiriki kilele cha maonesho hayo Rais Samia amesema kuwa, miongoni mwa Juhudi zilizofanywa kuboresha Kilimo ni pamoja na kuanzishwa kwa Programu ya Miaka 8 ya kujenga kesho Bora ya Vijana ijulikanayo kama Building Better Tomorrow (BBT) inayolenga kuhamasisha Vijana kufanya Kilimo Cha Kisasa kwa lengo ya kujikwamua kiuchumi kwa wao wenyewe na Taifa kwa ujumla.

Aidha, Mhe. Samia ametumia maadhimisho hayo kuelezea umati wa wananchi walioshiriki maonesho hayo na watanzania kwa ujumla kuwa kuwa Serikali yake haijazuia wananchi hususani Wakulima kuuza mazao nje ya Nchi Bali inawataka pawepo na utaratibu mzuri wa kusafirisha mazao hayp ikiwa ni pamoja na wakulima kuuza mazao yao kupitia kwa Wakala wa Taifa wa hifadhi ya chakula (NFRA) hatua itakayosaidia kuondoa uuzwaji wa mazao hayo kiholela nje ya nchi.

Katika hatua nyingine Rais Samia, ameielekeza Wizara ya Kilimo kuangalia uwezekano wa kutoa Maji kwenye maziwa na kuyapeleka kwa Wakulima kwaajili ya kusaidia Kilimo Cha Umwagiliaji ambapo itasaidia kwa Kiasi kikubwa kuongeza uzalisha wa chakula cha kutosha hasa katika maeneo yasiyopata mvua za kutosha kwa mwaka.

Kupitia maadhimisho hayo Rais Samia ameshuhudia utiaji Saini wa mikataba wa Mradi wa kujenga kesho Bora ya Vijana (BBT) baina ya Wizara ya Kilimo, Wizara ya mifugo na Uvuvi na Jeshi la kujenga Taifa (JKT) ambapo vijana hao watapata fursa ya kujengewa uwezo katika masuala ya Kilimo pamoja na kupewa elimu ya uzalendo kwa mwezi mmoja.

Mhe. Samia Suluhu Hassani amehitimisha kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Nanenane kwa kuzindua programu ya uchimbaji visima 67,800 kwa wakulima wadogo Nchi nzima, Ugawaji wa vishikwambi kwa maafisa ugani, utoaji wa vifaa vya kutengeneza Vihenge kwa wakulima nchi nzima, Makala ya Miradi ya Umwagiliaji, Usanifu wa uwanja wa Kisasa wa Maonesho ya Kilimo na kushuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya uendelezaji wa BBT kati ya Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Kwa upande wake Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Sarah Mwaipopo, amesema kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali za Serikali katika utatuzi wa migogoro ikiwemo migogoro yote inayohusiana na masuala ya ardhi.

Akizungumzia dhumuni la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kushiriki Maonesho hayo Mwaipopo amesema kuwa, ofisi yake imeshiriki maadhimisho hayo kwa kuwa ndio inasimamia masuala ya utatuzi wa migogoro na moja kati ya migogoro ambayo imejitokeza kwa Kiasi kikubwa ni pamoja na migogoro ya ardhi ambayo ndio inahusiana na madhumni hasa ya maonesho ya nanene kwa kuwa kwa mwaka huu yamejikita zaidi kwenye usalama wa chakula.

Ameongeza kuwa ili kuwa na chakula cha kutosha na chenye usalama ofisi yake itaendelea kutatua migogoro hiyo hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa chakula cha kutosha kwa kuwa uwepo wa migogoro ya ardhi nchini umechangia kwa Kiasi kikubwa kupunguza uzalishaji hasa wa chakula katika maeneo mbalimbali nchini.