Habari

Imewekwa: Jan, 23 2022

RAIS MWINYI: ZINGATIENI MAADILI NA SHERIA KATIKA UTOAJI HAKI:

News Images

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe, Dkt. Hussein Ali Mwinyi mapema leo amezidua maadhimisho ya Wiki ya Sheria na kuwakumbusha watumishi wa Mahakama ya Tanzania na wadau wote wa sekta ya sheria nchini umuhimu wa kuzingatia maadili katika utoaji haki na kuheshimu sheria hatua itakayosaidia kujenga umoja, amani na mshikamano ili kuhakikisha malengo waliyojiwekea yanatimia.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mhe. Mwinyi amebainisha kuwa kwa nafasi yake kama Rais wa Zanzibar, ambaye ameitumikia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ngazi mbalimbali ikiwemo uwaziri, anatambua na kuheshimu umuhimu wa sheria kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia anafahamu umuhimu wa sheria katika kujenga umoja, amani, udugu na mshikamano, hivyo mafanikio ya kiuchumi, kibiashara na kiuwekezaji hutegemea kuwepo kwa misingi imara ya utawala bora, sheria na uhuru wa Mahakama.

“Ni dhahiri kuwa ustawi wa wananchi wetu, kwa kiasi kikubwa unategemea kuwepo kwa sheria madhubuti zinazotambua ukweli kuwa wananchi wengi kutoka pande zote mbili za Muungano ni maskini. Hivyo, sheria zetu na taratibu za kimahakama ndizo zitakazosaidia kuwainua na kufanikisha shughuli zao kiuchumi na kijamii, kwa kuwa uwepo wa sheria bora zinazosimamiwa vyema ndio kutafanikisha uchumi wao, biashara na shughuli zao za kila siku za kujitafutia kipato,”amesema Dkt. Mwinyi.

Kiongozi huyo amesisitiza kuwa upo umuhimu wa kuheshimu sheria zetu kwa kuzingatia ukweli kuwa anatambua kuwa miongoni mwa mambo yanayodhoofisha misingi ya utawala bora ni kuwepo kwa vitendo vya rushwa, ubadhirifu, uzembe, ikiwa ni pamoja na kukosa uwajibikaji na kutofuata sheria hatua inayopelekea ukiukwaji kwa maadili.

“Nachukua fursa hii kupongeza jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Mahakama ya Tanzania katika kuimarisha huduma za kutoa haki kwa wananchi na kuhakikisha mnaongeza kasi ya kusikiliza mashauri mbalimbali yanayowasilishwa katika ngazi zote za Mahakama,” amesema Dkt. Mwinyi.

Rais Mwinyi amepongeza hatua ya kuanzisha Mahakama inayotembea kwa kuwa imesaidia kufikisha huduma ya utoaji haki kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini. Huku akipongeza hatua mbalimbali zilizochukuliwa ikiwemo kutafsiri sheria kwa lugha ya Kiswahili, jambo ambalo limewapa Watazania matumaini kama hatua mojawapo ya maendeleo ya sekta ya sheria nchini.

Aidha kiongozi huyo ameshauri kuongeza jitihada za kupata wataalam wa lugha ya alama pamoja na kuimarisha miundombinu inayozingatia uwepo wa Watanzania wenye mahitaji maalum, wakiwemo watu wenye ulemavu wa aina tofauti hatua itakayosaidia makundi maalum kupata haki zao bila kikwazo chochote.

Akizungumzia kuhusu ya ushirikiano iliyopo baina na Mahakama ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mahakama ya Zanzibar. Rais Mwinyi ameelezea kuridhishwa na ushirikiano uliopo huku akiwasihi kuuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa mapana ya Taifa.

“Nimeelezwa kuwa uhusiano huo ni wa muda mrefu toka mwaka 1965, nafurahi kuona kuwa ushirikiano huo unaendelezwa kwa kupeana uzoefu na utaalam utakaoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yenu. Natoa wito kuendeleza ushirikiano huo kwa lengo la kuwa chachu ya kuleta mabadiliko ya utendaji na kuongeza kasi na ufanisi katika Mahakama zetu,” alisema.

Mhe. Dkt Mwinyi amepongeza mafanikio makubwa aliyoyaona wakati akitembelea maonesho yaliyoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho ya Wiki ya Sheria, ambapo ameelezwa kuwa huduma zitakazotolewa kwa siku zote za maonesho ni moja ya utekelezaji wa nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama na malengo makuu ya nguzo hiyo ni pamoja na kuimarisha imani ya wananchi na kuongeza uelewa na ufahamu wao wa taratibu na shughuli za utoaji haki nchini.

Katika hatua nyingine Rais Mwinyi amekubaliana na uamuzi wa kuzidi kutoa taaluma kuhusu huduma za Mahakama kwani bado haijawafikia wananchi walio wengi. Amebainisha kuwa ni wazi wananchi watanufaika na huduma hiyo, hivyo ametoa wito kwa wananchi wote kuitumia fursa iliyopo vizuri kwa kufika kwa wingi kwenye maonesho hayo.

“Kupitia maenesho haya pia nimeshuhudia uboreshaji makubwa unaofanywa na unaoendelea kufanywa katika mnyororo mzima wa utoaji haki. Ni dhahiri kuwa uboreshaji mkubwa niliyoshuhudia ya matumizi ya TEHAMA ni dalili njema ya matayarisho makubwa ya kupokea na kuendeleza matumizi ya TEHAMA ndani ya Mahakama zetu. Natoa pongezi za kipekee kwa uongozi wa Mahakama ya Tanzania na watumishi wote kwa kuendeleza uboreshaji huu mkubwa,” amesema.

Mhe. Dkt Mwinyi pia alitumia fursa hiyo adhimu ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria kutoa wito kwa wanasheria na wataalam wote wa sheria, viongozi wa Mahakama na Watumishi wote wa sekta ya sheria kuielewa na kuifanyia kazi mipango mikuu ya uchumi inayotekelezwa na Serikali zote mbili nchini katika jitihada za kupunguza umasikini na kuwa na uchumi unaolingana na ushindani wa karne ya 21, hivyo kuwa huru kutoa ushauri wao wa kisheria kwa lengo la kuifanikisha.

Ameeleza kuwa anatambua kuwa zipo sheria ambazo huenda zikawa ni kikwazo cha kufikia matarajio yetu ya kiuchumi na hasa uchumi wa bluu na ustawi wa jamii, hivyo Sheria hizo zitahitaji kufanyiwa marekebisho ili zifanikishe mipango yetu ya uchumi wa kisasa hivyo naomba tumieni utaalam wenu kuzishauri Serikali zetu kuchukua hatua za kurekebisha sheria ambazo zinakasoro, nasi tutafanya hivyo kwa maslahi mapana ya nchi yetu na Watanzania wote.

Maadhimisho ya Wiki ya Sheria nchini yamezinduliwa leo Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali yakiwa na kauli mbiu isemayo Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho kuelekea Mahakama Mtandao.