Habari
PROF. KABUDI: TUNA DENI KUBWA KWA WATANZANIA
Tuna deni kubwa kwa watanzania wa kawaida la kuwahudumia na kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Palamaghamba Kabudi alipowasili Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Dar es Salaam baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam kushika nafasi hiyo.
“Tuna deni kubwa kwa watanzania wa kawaida katika Sekta ya Sheria ambapo tumepewa dhamana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuhudumia wananchi kwa kuwa kazi ya kuongoza nchi siyo kazi ndogo na wanasheria tuna nafasi kubwa ya kulifanya taifa lisimame au lidodondoke, tunatakiwa kusaidia mhimili wa Mahakama,’’ amesema Prof. Kabudi.
Ameongeza kuwa tumepewa jukumu kubwa la kumsaidia Mhe. Rais Dkt. Samia kutoa huduma kwa wananchi ambapo tunatakiwa tufanye matendo mema kwa wengine kwa mujibu wa Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia kwa hisani aliyotupa kututeua katika nafasi mbali mbali za Sekta ya Sheria na kutupa dhamana hii. Pamoja na Prof. Kabudi, viongozi wengine wa Sekta ya Sheria walioteuliwa na kuapishwa na Mhe. Rais Dkt. Samia ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Franklin Rwezimula, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Saleh Possi, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel Maneno na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi.
Pia, amewashukuru na kuwapongeza viongozi wote waliohudumu katika nafasi mbali mbali kwa kazi kubwa waliyoifanya ambapo nafasi hizo wamepewa wengine na viongozi hao ni Dkt. Boniphace Luhende aliyekuwa Wakili Mkuu wa Serikali na Jaji Dkt. Elizer Feleshi aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na sasa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Hafla hiyo ya ukaribisho baada ya uapisho imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Jumanne Sagini, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Eliakim Maswi, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo, baadhi ya viongozi wa Wizara hiyo na taasisi zake, Menejimenti na watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.