Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

OSG YAPUNGUZA GHARAMA KWA WADAU YA KUPATA USHAURI WA KISHERIA

Imewekwa: 25 July, 2025
OSG YAPUNGUZA GHARAMA KWA WADAU YA KUPATA USHAURI WA KISHERIA

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) yapunguza gharama kwa wadau wa karibu ya kupata ushauri mbali mbali wa kisheria kwa wadau ambao wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kutoka mkoa wa Tabora kwenda mikoa mingine kupata ushauri wa kisheria.

Hayo yameelezwa na Kaimu Wakili wa Serikali Mfawidhi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Mkoa wa Tabora, ndugu Gureni Mapande wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo alipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa Mawakili wa Serikali wa Ofisi hiyo mkoani Tabora.

Mapande alisema kuwa, “OWMS Tabora imefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi mathalani mdau anayekusudia kuishtaki Serikali hatumii gharama za kusafiri kwenda mikoa mingine kupeleka notisi ya kusudio la kuishtaki Serikali bali notisi hiyo inawasilishwa na OWMS Tabora.”

Akiwa ziarani mkoani humo Bi. Mtulo alisema kuwa lengo la ziara yake ni kukagua utendaji kazi wa Ofisi hiyo kwenye mikoa mbali mbali ikiwemo mkoa wa Tabora ikiwemo namna Mawakili wa Serikali wa Ofisi hiyo wanavyoendesha mashauri kwa niaba ya Serikali, ushirikiano wa Mawakili hao na wadau wa OWMS ikiwemo mahakama, halmashauri mbali mbali na taasisi nyingine za Serikali ili OWMS iweze kubaini uhalisia, kupata changamoto, kuona mazingira ya utendaji kazi, kupata maoni na kuyafanyia kazi ili kuboresha utendaji kazi wa OWMS.

Pia, Bi. Mtulo alikutana na Mawakili wa Serikali wa Halmashauri za Mkoa wa Tabora na kutoa rai kwao ya kuhakikisha wanashiriki vikao na majukumu yao yanayohusu masuala ya kisheria yanayotekelezwa kwenye halmashauri zao na wawasilishe changamoto wanazokutana nazo kwa viongozi wa maeneo yao na kwa Mawakili wa Serikali wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye Ofisi za Mikoa hususani changamoto zinazohusu uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi ili yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati.

Aidha, Bi. Mtulo aliwaeleza Mawakili wa Serikali wa Halmashauri hizo kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imewapa kibali Mawakili wa taasisi za Serikali Mawakili wa Serikali waliopo kwenye halmashauri zote nchini kuendesha mashauri kwa niaba ya Serikali hivyo watumie vibali hivyo kuendesha mashauri hayo kwenye maeneo yao.

Naye Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Mhe. Dkt. Frank Mirindo amempongeza Bi. Mtulo kwa kufanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa Ofisi hiyo kwenye mkoa wa Tabora na amemweleza kuwa Mawakili wa Ofisi hiyo wanafika mahakamani kwa wakati na kuendesha mashauri vizuri kwa niaba ya Serikali.