Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

OSG YAPONGEZWA KUFUNGUA OFISI, YASOGEZA HUDUMA KWA WANANCHI

Imewekwa: 24 July, 2025
OSG YAPONGEZWA KUFUNGUA OFISI, YASOGEZA HUDUMA KWA WANANCHI

Mahakama ya Tanzania imeipongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kufungua Ofisi kwenye mkoa wa Manyara ili kusogeza huduma karibu na wadau na wananchi ya uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake

Hayo yameelezwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala Ndogo ya Manyara, Mhe. Devotha Kamuzora wakati wa ziara ya Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo alipofika mahakamani hapo.

Mhe. Jaji Kamuzora amesema kuwa ufunguzi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwenye mkoa huo ni jambo zuri kwa kuwa wamesogeza huduma karibu na wadau na wananchi wanaowahudumia kwa kuwa hapo awali Mawakili wa Serikali wa Ofisi hiyo walikuwa wanatoka mkoa wa Arusha kuja Manyara kuendesha mashauri kwa niaba ya Serikali na taasisi zake hivyo kupelekea ucheleweshaji wa usikilizaji wa mashauri hayo.

“Ufunguzi wa Ofisi Manyara umerahisisha na kuharakisha uendeshaji wa mashauri kwa kuwa Mahakama kuu Kanda ya Manyara tumejiwekea malengo ya kuendesha na kumaliza shauri kwa muda usiozidi miezi sita. Hivyo, ziara yako ya kutembelea Ofisi inakupa picha halisi na kuboresha mazingira ya kazi ili Mawakili waweze kuwahudumia vizuri wadau,” alifafanua Mhe. Jaji Kamuzora.

Bi. Mtulo alisema kuwa lengo la ziara yake ni kukagua utendaji kazi wa Ofisi hiyo na kujua changamoto wanazokabiliana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kama Mawakili wa Serikali. Aidha, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali ameshuhudia namna Ofisi ya Mkoa huo inavyoendesha mashauri kwa wakati kwa kushirikiana na Mahakama na Mawakili wengine wa taasisi za Serikali.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, Mhe. Bernard Mpepo amewapongeza Mawakili wa Serikali wa Mkoa wa Manyara wanaofanya kazi na Mahakama hiyo kwa kutoa ushirikiano kwa Majaji na Mawakili wengine wa taasisi za Serikali kuendesha mashauri ya Serikali na kusogeza huduma karibu na wananchi wa mkoa wa Manyara.