OSG YAJIPANGA UENDESHAJI WA MAJUKUMU YA KISHERIA
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yafanya tathmini ya utendaji kazi katika kipindi cha nusu Mwaka wa Fedha 2025/26 na kujipanga kutekeleza majukumu yake katika kipindi cha mwezi Januari, 2026 hadi Juni, 2026.
Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi ameendesha kikao cha menejimenti cha kutathmini utendaji kazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kilichofanyika jijini Dodoma kwa lengo la kuchambua taarifa ya utekelezaji ya Ofisi hiyo, kupanga mikakati mipya ya utendaji kazi ili kuhakikisha kuwa Ofisi hiyo inaendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa tija na ufanisi ndani na nje ya nchi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake.
“Kikao hiki ni cha kimkakati, lengo ni kujipanga kuendesha majukumu ya kisheria ya Ofisi ikizingatiwa kuwa kikao hiki kinafanyika kuelekea Siku ya kilele cha Wiki ya Sheria inayoadhimishwa kila mwaka mwanzoni mwa mwezi Februari, 2026,” amesisitiza Dkt. Possi.
Pia, Dkt. Possi ameongeza kuwa Ofisi imedhamiria kufungua Ofisi nyingine kwenye mikoa ya Katavi, Geita, Singida ili kusogeza huduma karibu na wananchi na amewataka wajumbe wa menejimenti ya Ofisi hiyo kuendelea kutumia mifumo ya TEHAMA katika utendaji kazi.
Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo akizungumza kwa niaba ya menejimenti ya Ofisi hiyo amemhakikishia Dkt. Possi kuwa kwa kuwa mwaka mpya umeanza na Ofisi inaingia kipindi cha pili cha Mwaka wa Fedha, wajumbe wa menejimenti hiyo wataendelea kutekeleza majukumu kwa wakati.
Kikao hicho hufanyika mara moja kwa mwaka ili kuwapa muda wa kutosha wajumbe wa menejimenti wa Ofisi hiyo kutoa taarifa ya utendaji kazi na majukumu yaliyopangwa kutekelezwa kwa kipindi cha pili cha Mwaka wa Fedha 2025/26.