Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI YASHIRIKI UFUNGUZI WA MAONESHO YA NANENANE

Imewekwa: 05 August, 2025
OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI YASHIRIKI UFUNGUZI WA MAONESHO YA NANENANE

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi na wadau wake hatua ambayo imesaidia kwa kiasi kikubwa kusogeza huduma karibu na wananchi na wadau wake.

Huduma hii inatolewa bure kwa wananchi wote wanaofika kutembelea banda la ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali lililopo ndani ya viwanja vya nanenane vilivyopo jijini Dodoma yanapofanyika Maonesho ya Nanenane Kitaifa.

Kupitia Maonesho hayo, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali itaendelea kuwajengea uelewa wananchi wanaotembelea banda lake kuhusu masuala ya kisheria ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi ikiwemo masuala ya ardhi, ajira, haki za binadamu na mikataba.

Aidha, wakati wa Maonesho hayo wadau watakaotembelea banda hilo wataendelea kujengewa uelewa kuhusu jukumu kuu la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, ambalo ni Kusimamia, kuratibu na kuendesha mashauri yote ya madai, usuluhishi, katiba, haki za binadamu na uchaguzi yanayofunguliwa dhidi ya Serikali na Taasisi zake ndani na nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa kufungua Maonesho hayo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewasihi viongozi kutambua wajibu walionao katika kutekeleza dira ya maendeleo ya Taifa 2050 na mipango ya maendeleo ya sekta ya kilimo na taifa kwa ujumla. Aidha, ipango hiyo,imedhamiria kuongeza kasi ya ukuaji wa kilimo hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka, ifikapo 2030.

Ameongeza kuwa, ni vyema kila kiongozi kuwajibika kwa kuwaelekeza wakulima, wafugaji na wavuvi kuweka nguvu zaidi kwenye mazao yenye thamani kubwa sokoni, kuwekeza katika uzalishaji wa kisasa ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje, kuvutia wawekezaji wa ndani na nje pamoja na kuwekeza katika miundombinu baridi ya uhifadhi na usafirishaji.

Aidha, Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango ametoa wito kwa viongozi kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wasindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kuhusu fursa zilizopo za kupata mitaji kutoka kwenye benki na taasisi nyingine za fedha ambazo tayari zinatoa mikopo nafuu kwa ajili ya kilimo-biashara. Hatua hiyo itawawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kiuchumi hususan katika upatikanaji wa mitaji, teknolojia, elimu na mafunzo pamoja na upatikanaji wa huduma za ugani ikiwemo kukuza matumizi ya kanuni bora za kilimo. Hii itahamasisha maendeleo ya ushirika na ushirikiano kati ya wakulima, wafugaji, wavuvi na watafiti, maafisa ugani na watunga sera nchini.

Mhe. Dkt. Mpango amesema kuwa ni wajibu wa kila kiongozi kuhimiza wananchi kutumia mbinu zinazoweza kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia ya nchi na changamoto nyingine zinazowakumba wakulima ikiwemo kuhimiza matumizi bora ya ardhi, kushawishi wananchi kupanua mawanda ya kilimo na kuhimiza zaidi kilimo cha mazao yanayohimili ukame nchini.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mpango amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya kilimo nchini yametokana na juhudi mbalimbali za wakulima, wafugaji, wavuvi, wadau wa maendeleo, pamoja na jitihada mahususi za Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kukuza sekta hiyo nchini.

Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango amezitaja jitihada hizo kuwa ni ongezeko la bajeti za Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi, pamoja na sekta nyingine saidizi ambapo kwa mwaka wa fedha 2025/26 Wizara ya kilimo imetengewa shilingi trilioni 1.243, ikilinganishwa na shilingi bilioni 229.99 iliyotengwa mwaka 2024/25.

Maonesho ya Nanenane kwa mwaka 2025 yanaongozwa na Kaulimbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025” yaliyoanza terehe Mosi hadi 08 Agosti 2025. Kaulimbiu hii imechaguliwa mahsusi ili kukumbusha umuhimu wa viongozi bora katika kuinua uzalishaji kwenye kilimo, ufugaji na uvuvi, hasa katika kipindi hiki ambapo nchi yetu inaelekea kufanya uchaguzi Mkuu, baadae Oktoba 2025.