Habari

Imewekwa: Nov, 12 2021

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yapata hati safi

News Images

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imefanikiwa kupata Hati Safi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 ikiwa ni mara ya pili mfululizo hali ambayo imesababishwa na nidhamu ya matumizi ya fedha Pamoja na ushirikiano baina ya watumishi na menejimenti ya Ofisi hiyo.

Hayo yamesemwa na Mhasibu Mkuu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Devotha Ngulungulu alipokuwa anazungumza na waandishi wa Habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Alisema upatikanaji wa hati safi umetokana na jitihada zinazofanywa na watumishi wa ofisi hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na menejimenti hususani katika kusimamia vizuri Rasilimali za ofisi katika idara na vitengo vyote za taasisi hiyo.

“Tulianza kuandaa bajeti, mpango kazi mpaka kuandaa taarifa ya fedha ya mwaka na tulifanya hivyo kwa ushirkiano wa idara zote jambo ambalo lilitufanya tupate hati safi kwa mara ya pili”, alisema Ngulungulu.

Alisema taarifa ya fedha iliyokuwa imeandaliwa na Ofisi hiyo ilimridhisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutokana na kuzingatia viwango vya uandaaji wa hesabu kwa mwaka husika na hivyo kumfanya kutoa hati safi kwa OWMS.

Ngulungulu alisema katika ukaguzi uliofanywa na CAG ilibainika kwamba ofisi inazingatia vizuri sheria za manunuzi na usimamizi mzuri wa fedha hali ambayo ilichochea kupatikana kwa hati hiyo.

Ngulungulu alisema Ofisi hiyo itaendelea kuzingatia sheria za fedha, taratibu za manunuzi Pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia mpango kazi wa mwaka husika katika idara zote ili kuepuka ukiukwaji wa Sheria za fedha utakaosababisha hoja za ukaguzi.

“Sasa hivi tumejipanga kuendelea kutoa elimu kwa watumishi wasiokuwa wahasibu juu ya matumizi ya sheria za manunuzi na matumizi bora ya mifumo ya fedha ili kufuta hoja za ukaguzi, ikiwezekana tunataka tusiwe na hoja kabisa,” alisema Ngulungulu

Mhasibu Mwandamizi wa Ofisi hiyo, Motte Massima alisema kupata Hati Safi katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kunaashiria uwajibikaji wa idara zote kuanzia menejimenti na uwezo wa watumishi katika kitengo cha uhasibu.

Aliongeza kuwa watumishi wa kitengo cha hicho wamepatiwa mafunzo mbalimbali yanayowawezesha kuandaa vizuri hesabu za Serikali na hivyo kusaidia kuepuka utengenezaji wa hoja.

Massima amesema kitendo cha taasisi yoyote kupata hati safi kinaifanya kuaminika na Serikali Pamoja na wafadhili kutokana na kuwa na uhakika wa fedha zinazotolewa kutumika vizuri hatua inayosaidia serikali kuweza kupata fedha kutoka kwa wahisani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.