Ofisi ya Wakili MKuu wa Serikali yaokoa Shilingi Bilioni 602.5
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikiwa ndio yenye dhamana ya kusimamia, kuratibu na kuendesha mashauri ya Madai na Usuluhishi ndani na nje ya nchi imeokoa jumla ya Sh bilioni 602.52, dola za kimarekani milioni 800.2 na euro milioni mbili ambazo serikali ingetakiwa kulipa kama serikali ingeshindwa katika mashauri mbalimbali yaliyofunguliwa ndani na nje ya nchi.
Hayo yamezungumzwa leo tarehe 10 Oktoba 2024 na Wakili Mkuu wa Serikali na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi wakati akifungua Mkutano wa kwanza wa Baraza la pili la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali uliofanyika mkoani Dodoma.
Kiongozi huyo amesema kuwa Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 536.5 zilizookolewa na ofisi hiyo ni fedha ambazo zingelipwa na serikali kwa wadai mbalimbali waliofungua mashauri dhidi ya serikali katika mahakama za ndani na nje ya nchi, Wakati Sh bilioni 66.02, dola milioni 800.2 na euro milioni mbili ni fedha zilizookolewa baada ya kumalizika mashauri hayo kwa njia ya majadiliano nje ya mahakama.
Kuhusu uendeshaji wa mashauri Dkt. Possi amesema kuwa Katika mwaka wa fedha 2023/24, Ofisi imesajili na kuendesha jumla ya Mashauri ya madai takribani 9,650 kati ya Mashauri hayo, Mashauri 9,519 ni ya kitaifa (zaidi ya asilimia 60 ni mshauri ikiwa ni migogoro ya ardhi) na Mashauri 131 ni ya kimataifa. Katika kuendesha Mashauri hayo, Mashauri 1,412 yalimalizika, na kufanikiwa kuokoa jumla ya shilingi za kitanzania Bilioni Mia Tano Thelathini na Sita na Nukta Tano (536,515,717,327).
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho hicho, cha Mwaka wa fedha 2023/24, Ofisi imeshughulikia jumla ya Mashauri ya usuluhishi 201 ambapo, kati ya Mashauri hayo, Mashauri 170 ni ya usuluhishi wa ndani na Mashauri 31 ni ya usuluhishi wa kimataifa. Kati ya Mashauri 201 yaliyoshughulikiwa, Mashauri 43 yamemalizika kwa njia ya majadiliano, mahakamani na kwenye Mabaraza ya Usuluhishi na kufanikiwa kuokoa jumla ya shilingi Bilioni Sitini na Sita nukta Sifuri Mbili (66,020,015,593.38), Dola za Marekani Milioni Mia Nane Nukta Mbili (817,643,693.12) na EURO Milioni Mbili (2,000,000).
Dkt. Possi ameeleza katika kiindi husika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali iliata mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na Kuiwakilisha Serikali na Taasisi zake kwa ufanisi katika mashauri ya Madai na Usuluhishi ndani na nje ya nchi ambapo katika kutekeleza jukumu hili, Ofisi imeweza kuokoa fedha mbalimbali ambazo Serikali ingetakiwa kulipa iwapo ingeshindwa katika mashauri hayo.
Aidha, Ofisi imeendelea kuongoza na kushiriki katika Timu za Serikali za Majadiliano (GNT) na kufanikisha kumaliza mashauri/migogoro nje ya Mahakama, na kufanikiwa kuisaidia Serikali kuokoa kiasi tajwa hao juu fedha ambazo sasa zitaelekezwa kwenye miradi mikubwa ya kimkakati inayojengwa nchi nzima kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Akieleza kuhusu mikakati mbalimbali iliyowekwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa mwaka 2024/25, kiongozi huyo ameeleza kuwa ofisi yake imeweka mikakati mbalimbali ambapo ofisi yake itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wake ili kuweza kuwajengea mazingira bora yatakayosaidia kutekeleza majukumu yao na kufikia malengo yao waliyojiwekea kwa wakati.
Aidha, ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, imepanga kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wake kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa watumishi wa ofisi hiyo, hatua itakayowasaidia kuwa wabobezi katika uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhushi, kujadiliana na kushauriana ili kuboresha usimamizi wa mashauri ya madai ndani na nje ya nchi.
Katika mkutano huo wa siku mbili, Wakili Mkuu wa Serikali amesema kuwa katika siku ya pili wajumbe wa baraza hilo, watapata mafunzo mbalimbali yakiwemo ya mafunzo kuhusu
Masuala ya Udhibiti wa Msongo wa Mawazo, elimu juu ya maandalizi ya kustaafu, dhana ya Ujumuishi wa Anuai za Kijamii (Workforce Diversity and Inclusion) sehemu za kazi.
Katika hatua nyingine Dkt. Possi amewahimiza wajumbe hao na wananchi kote nchini kushiriki kikamifu kujiandikisha kwenye daftari la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kushiriki uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwezi novemba 27, mwaka huu, na kushiriki kikamilifu kupiga kura katika uchaguzi Mkuu mwakani ili waweze kutumia haki yao ya kikatiba ya kuwachagua viongozi wanaowataka ili waweze kuwaletea maendeleo.
Awali Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo amewataka watumishi wa ofisi hiyo kuendelea kuchapa kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa Umma ili waweze kudumisha maslahi na taswira ya ofisi yao na kufikia malengo wakiyojiwekea kwa wakati.
Bi. Amesema kuwa kati ya Julai 2023 hadi Juni 2024, watumishi 80 wamepata mafunzo ndani na nje ya nchi, pamoja na kuboresha ofisi kwa kuweka vifaa 69 vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.