Habari

Imewekwa: Jan, 22 2024

OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI YAMALIZA MASHAURI YENYE MASLAHI MAPANA KWA TAIFA

News Images

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) imefanikiwa kumaliza mashauri yenye maslahi mapana kwa taifa kwa kusimamia na kuendesha mashauri ya madai, usuluhishi, katiba, haki za binadamu na uchaguzi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake ndani na nje ya nchi ambapo mafanikio hayo yamejikita kwenye mashauri yenye maslahi mapana kwa taifa.

Hayo yameelezwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende wakati wa mafunzo ya uongozi na kikao cha faragha kwa wajumbe wa Menejimenti wa Ofisi hiyo wakati akimkaribisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi kuzungumza na wajumbe wa Menejimenti wa Ofisi hiyo leo tarehe 17 Januari, 2024 Kibaha, Pwani

“Hadi kufikia mwezi Septemba, 2023; OWMS imeendesha jumla ya mashauri 7,393 ya madai na usuluhushi ambapo imefanikiwa kumaliza mashauri yenye maslahi mapana kwa taifa ambayo ni pamoja na shauri la urejeshaji wa ndege ya Serikali nchini; uwekezaji wa kampuni ya DP World; kumaliza shauri la kampuni ya madini ya Winshear kwa njia ya majadiliano ambapo Serikali imelipa dola za marekani milioni 30 badala ya dola za marekani milioni 120 na kuokoa dola za marekani milioni 90; kampuni ya Tanga Cement dhidi ya kampuni ya Twiga Cement; na kumaliza shauri la kuongezewa muda wa utumishi wa Jaji Mkuu,” amefafanua Dkt. Luhende

Ameongeza kuwa wajumbe hao wanapatiwa mafunzo ya uongozi pamoja na mada kuhusu uwekezaji na namna ya kuongeza kipato; mfumo wa mashauri wa Mahakama Kuu; mashauri ya haki za binadamu; maadili ya viongozi; udhibiti ubora; mifumo ya TEHAMA; afya ya akili na saikolojia

Akizungumza kwa wajumbe wa OWMS wakati wa mafunzo hayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi alisema kuwa OWMS ni Ofisi kubwa na haina mbadala kwa kuwa imebeba dhamana ya nchi.

“Wanaofanya kazi na OWMS, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka lazima uaminike, tuepuke matatizo yanayoweza kuathiri utendaji kazi wetu na tuzingatie maadili ya utumishi wa umma na miiko ya taaluma zetu,” amesisitiza Dkt. Feleshi

Dkt. Feleshi ametoa rai kwa Mawakili wa Serikali kuzingatia masuala kumi yafuatayo katika utekelezaji wa majukumu ambayo ni kujifunza maarifa na stadi mpya za kazi; kuandaa dondoo za mawasilisho na marejesho wa kazi ulizofanya; kuwa na mawasiliano na mahusiano yenye tija na wenzako au wadau; kutotenda jambo lililo juu ya maelekezo uliyopewa; kuwa mwangalifu katika maneno au mawasiliano unayofanya; kujilinda na uovu na kuwa mwaminifu muda wote kama kuna jambo baya umefanya toa taarifa mapema; kuwa tayari wakati wowote kwa uwakilishi na kutoacha ombwe la uwakilishi pale shauri na Serikali linapotokea halina Wakili husika; kuwajengea uwezo wa kazi wenzako kwa kutekeleza jukumu ulilopewa kwa kuwasaidia, kusimamia na kuwawezesha; na kufanya utafiti bila kukoma

Naye Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Mark Mulwambo alisema kuwa mafunzo ya uongozi yametolewa kwa wajumbe wa OWMS ambapo yanajumuisha ushiriki wa Wakuu wa Idara, wakuu wa Vitengo na Mawakili wa Serikali Wafawidhi wa Mikoa wa OWMS kutoka mikoa 17 ambapo mafunzo hayo yatawawezesha kufanya tathmini ya utekelezaji wa makujumu, kuboresha, na kupanga vipaumbela na malengo ya OWMS kwa mwaka 2024