Habari

Imewekwa: Nov, 24 2022

OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI, TAASISI YA USULUHISHI TANZANIA KUSHIRIKIANA

News Images

Wakili Mkuu wa Serikal, Dtk. Boniphace Luhende ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Taasisi ya Usuluhishi Tanzania (Tanzania Institute of Arbitrators) kwa lengo la kuhakikisha Sekta ya Usuluhishi nchini inaimarika zaidi.

Dkt. Luhende ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na Rais wa Taasisi ya Usuluhishi Tanzania, Bi. Madeline alipomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujitambulisha na kujadiliana namna ya kuendeleza ushirikiano baina ya Ofisi hizo katika tasnia ya usuluhishi nchini kwa kuwa wanategemeana katika utendaji kazi.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Dkt. Luhende amempongeza Bi. Kimei kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya ya kuendeleza Taasisi hiyo kwa kushirikisha wadau waili waweze kupata haki stahiki kwa njia ya usuluhishi nchini na Ofisi yake iko wazi muda wote kwa ajili ya kuboresha Sekta ya Usuluhishi ili iweze kusonga mbele.

Pia, ameongeza kuwa Serikali ni mdau mkubwa wa Sekta hii nchini na jambo hili linajidhihirisha kwenye bajeti ya Serikali ambapo kwa asilimia kubwa bajeti hiyo inakwenda katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kwenye maeneo mengine kama vile ujenzi ambako kunazalisha migogoro wakati wa utekelezaji wake.

Amefafanua kuwa migogoro hiyo inapotokea inaleta haja ya uwepo wa usuluhishi badala ya kesi hizo kuingia kwenye mfumo wa Mahakama hivyo ni muhimu wakati wa usuluhishi kutengeneza mazingira ya kuona migogoro inamalizwa kwa wakati, haraka, na kwa kutumia gharama nafuu.

“Kumekuwa na gharama za uendeshaji wa migogoro hiyo kwa kuwa usuluhishi unachukua muda mrefu hivyo kuongeza gharama kwa wahusika na nia yetu ni kuhakikisha kuwa ushirikiano wetu unaenda kupunguza gharama hizi,” alisema Dkt. Luhende.

Amesisitiza kuwa ni muhimu wasuluhishi wa migogoro wawe watu wenye taaluma husika, weledi, ujuzi, maadili, wazingatie kanuni za usuluhishi, walinde taswira ya taasisi husika, waepuke maslahi binafsi, wajenge imani ya taasisi kwa wadau na kulinda taswira yake katika uendeshaji wa migogoro mbali mbali kwa njia ya usuluhishi.

Kwa upande wake Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Sarah Mwaipopo amemshukuru Rais wa taasisi hiyo na amesisitiza kuwa ni muhimu kuwa vinara kwenye eneo la usuluhishi na Ofisi iko tayari kushirikiana na Taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuendeleza ushirikiano uliokuwepo tangu ulipoanzishwa na watangulizi wa Ofisi hizo ikiwemo kutenga rasilimali fedha kwa ajili ya uendeshaji mashauri ya usuluhishi, mafunzo kwa Mawakili ikiwemo Kanuni mpya za usuluhishi za mwaka 2022 ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Naye Rais wa Taasisi ya Usuluhishi Tanzania, Bi. Madeline Kimei amesema kuwa amefurahi kuona Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ina Idara ambayo imejikita kwenye masuala ya usuluhishi ambayo inafanikisha utoaji huduma za usuluhishi nchini na Taasisi hiyo iko tayari kushirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kujenga ujuzi kwa Mawakili waliopo nchini ili wote kwa pamoja waweze kufikia kiwango cha kimataifa cha uendeshaji wa usuluhishi

Katka hatua nyingine Mkurugenzi wa Idara ya usuluhishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, ndugu George Mandepo amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa Ofisi hii eneo la usuluhishi lilihusika na masuala ya ujenzi ila kwa sasa mwelekeo umebadilika katika muktadha wa usajili, uendeshaji, taratibu, kanuni, ada, usajili, maadili na nidhamu ambapo inagusa maeneo mbali mbali ya usuluhishi hivyo ni muhimu kuwe na uwazi na uwajibikaji katika tasnia ya usuluhishi ikiwemo kurithishana madaraka na kujenga uwezo kwa wasuluhishi chipukizi ili kulinda na kujenga taswira ya nzuri ya wasuluhishi, taasisi na wadau wanaohusika