Habari

Imewekwa: Nov, 07 2019

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali awapa somo Mawakili wa Serikali

News Images

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Gabriel Malata ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali kuendelea kujibidisha katika kujisomea machapisho mbalimbali ya kisheria kwa lengo la kujiongezea uwezo juu ya mambo mbalimbali yanayoihusu kada ya sheria.

Mhe. Malata ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam wakati akiendesha kikao na mawakili hao kwa lengo la kujadili mambo mbalimbali pamoja na changamoto wanazokutana nazo wakati wakitekeleza majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Mhe. Malata amesema, ni muhimu kwa Wakili wa Serikali kujijengea tabia ya kujisomea machapisho mbalimbali ya kisheria kwani kwa kufanya hivyo itamsaidia wakili kuwa na uwanja mpana hususani katika masuala yote yanayohusiana na namna ya uendeshaji wa mashauri Mahakamani.

Aidha, ameongeza kuwa kufanya maandalizi ya kutosha kwa Mawakili hao kutaisaidia Serikali kushinda kesi nyingi zilizopo Mahakamani hatua itakayopelekea kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kitakacho saidia kuboresha miundombinu na huduma nyingine za kijamii ili kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

Vilevile, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali amewaasa mawakili hao kuwa wanyenyekevu pindi wanapokuwa mbele ya majaji kwani unyenyekevu ndio sifa halisi ya Wakili wa Serikali.

Wakili wa Serikali lazima uwe mnyenyekevu (humble) hata lugha yako lazima ijitofautishe na za watu wengine, hata uvaaji wako lazima uwe nadhifu,” alisema Mhe. Malata.

Ili kuepusha mikanganyiko inayoweza kujitokeza Mahakamani, Mhe. Malata alisema kuwa ni muhimu kwa Wakili wa Serikali kupangilia hoja zake, hasa anapokuwa anaelezea zile hoja za msingi ili aweze kueleweka kirahisi hususani kwa majaji hatua itakayoiwezesha Serikali kushinda mashauri yote yaliyopo katika Mahakama mbalimbali za ndani na nje ya nchi.

Amebainisha kuwa ni vyema yakawepo mawasiliano mazuri baina ya Mawakili wa Serikali kwani kufanya hivyo itakuwa rahisi kwa watumishi hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, kwa kuwa mawasiliano mazuri yatawasaidia mawakili hao kuweza kusaidiana kwa wakati pale mmoja anapohitaji msaada wa haraka.

Amesema kuwa si vyema kwa Wakili wa Serikali kufanya kazi peke yake, hivyoamewataka kushirikiana ili waweze kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mambo mbalimbali hatua itakayosaidia kutekeleza kazi zao kwa weledi zaidi.

Unaweza ukakuta mtu anahangaika na jambo fulani, kumbe kuna mtu analifahamu jambo hilo kama ungewasiliana nae ingekuwa rahisi kulipatia ufumbuzi jambo hilo kwa wakati, alisema Mhe. Malata”.

Kuhusu mashauri ya uchaguzi kiongozi huyo amewaomba mawakili hao kuanza kujiandaa mapema ili waweze kuwa tayari kukabiliana na mashauri mbalimbali yatakayofunguliwa dhidi ya Serikali na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

Kiongozi huyo pia amewasihi mawakili hao kuwa waadilifu wawapo kazini kwani haitapendeza Wakili wa Serikali anakutwa akiwa anafanya mambo yasiyofaa kwa jamii kwa kufanya hivyo atapelekea kuipa sifa mbaya Ofisi ya Wakili Mkuu na Serikali kwa ujumla.

Amewasihi mawakili hao kutochagua mashauri ya kuendesha na kuwataka kuwa tayari kuendesha mashauri ya aina yote pasipo kujali yeye ni wakili kutoka idara ya Madai, Usuluhishi au idara ya Usimamizi wa Mashauri na Ubora,

Aliwataka mawakili hao kuhudhuria mashauri Mahakamani pale inapotokea wakili husika ameshindwa kufika Mahakamani hapo huku akisisitiza kuwachukulia hatua kali mawakili wote watakaoshindwa kuhudhuria Mahakamani kwa makusudi kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wameisababishia hasara Serikali.

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Mhe. Gabriel Malata amewapongeza mawakili hao na watumishi wote wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya katika kuhakikisha Ofisi hiyo inapiga hatua, huku akiwasihi kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi ili waweze kuisaidia Serikali ya awamu ya tano kupiga hatua katika Nyanja mbalimbali za kimaendeleo.