Habari

Imewekwa: Nov, 22 2021

JAJI MKUU AZINDUA VITABU VYA MKUSANYIKO WA MASHAURI YA MAHAKAMA YA KAZI

News Images

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mapema leo amezindua Vitabu vya Mkusanyiko wa Mashauri ya Mahakama ya Kazi (Labour Court Case Digest) ambapo amehimiza kasi ya usikilizaji wa mashauri na utatuzi wa migogoro ya kazi inayoletwa mahakamani ili kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi hapa nchini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Vitabu hivyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Jaji Mkuu amesema kuwa hakuna ubishi kwamba maendeleo ya mtu mmoja mmoja na kukua kwa uchumi wa nchi kwa ujumla kunategemea upatikanaji wa haki kwa wakati ambayo huchagizwa na umalizaji wa haraka wa migogoro inayowasilishwa Mahakamani.

Prof. Juma Amebainisha kuwa sekta ya kazi ni moja ya sekta muhimu katika ukuaji wa uchumu, hivyo kwa upekee, umalizaji wa haraka wa mashauri ya kazi yaliyopo katika ngazi mbali mbali za vyombo vya utatuzi wa migogoro ya kazi na utoaji haki ni moja ya nguzo muhimu katika ukuaji wa uchumi.

“Tulifanya Ugatuzi wa kuwapa mamlaka Majaji waliopo katika Kanda za Mahakama Kuu Ndio maana mnamo mwaka 2018, hatua hii iliwawezesha kusikiliza mashauri ya kazi. Hii imesaidia umalizikaji haraka wa mashauri ya kazi sehemu zote ambazo kuna Kanda ya Mahakama Kuu,” Jaji Mkuu alisema.

Kiongozi huyo wa juu wa Mahakama ya Tanzania ameongeza kuwa ili migogoro ya kazi iweze kutatuliwa kwa haraka na kwa wakati, ni sharti Mahakama itoe tafsiri ya sheria za kazi kupitia maamuzi mbalimbali ili kuwawezesha watatuzi wa migogoro kufanya maamuzi ya haki na kwa wakati.

“Vitabu hivi vitawezesha Mahakama na vyombo vingine vya kutoa haki katika sekta ya kazi pamoja na wadau wake kuleta urahisi wa rejea wakati wa usikilizaji na utoaji maamuzi wa mashauri ya kazi, pia vitabu hivi vitasaidia Waajiri na Wafanyakazi kujua zaidi mambo muhimu yaliyomo kwenye sheria za kazi kwa kuwa sheria hizo zimetafsiriwa katika vitabu hivi,” alisema.

Jaji Mkuu amesema kuwa Mkusanyiko wa vitabu hivyo utatusaidia kupunguza migogoro katika sehemu za kazi na kuchochea kuongeza ufanisi katika utendaji kazi kwa kila mmoja kujua haki na wajibu alionao utakaopelekea kukua kwa uchumi nchini kwetu.

“Kwetu sisi Mahakama ni chombo cha Usuluhishi na Uamuzi, hivyo kupitia vitabu hivi tutakuwa na nafasi nzuri ya kuongeza kasi ya usikilizaji wa mashauri na hivyo itawezesha wananchi kupunguza muda katika kudai haki na badala yake kutumia muda mwingi katika uzalishaji mali,” alisema Jaji Mkuu.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, Mhe. Salma Maghimbi alisema kuwa kwa mujibu wa kanuni ya 3(1)(a) ya Kanuni za Mahakama ya kazi, Mahakama hiyo inajukumu la kuweka kumbukumbu za maamuzi inayokuwa imeyatoa katika kutekeleza mamlaka yake, hivyo utekelezaji wa jukumu hilo ndilo chimbuko la kuwa na vitabu hivyo vya ripoti ya maamuzi ya Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi.

Akifafanua zaidi, Mhe. Maghimbi alisema kuwa “Labour Court Case Digest” ni vitabu vinavyokusanya maamuzi mbalimbali yanayohusiana na ajira na mahusiano kazini, yaliyoamuliwa na Majaji wa Divisheni ya kazi na mashauri hayo hukusanywa kwa umahiri ili kujumuisha maamuzi yanayogusa masuala tofauti na yenye kutoa tafasiri na misimamo ya Sheria za kazi, Kanuni zilizopo pamoja na Mikataba ya Kimataifa inayohusiana na masuala ya kazi.

“Ukusanyaji huu hufanywa na watalaamu waliobobea katika Sheria na uwezo wa kufanya uchambuzi wa mashauri, kuyakusanya na kuyaripoti kwa namna ambayo itamnufaisha mlengwa,” alisema Mhe. Maghimbi

Aidha, alibainisha kuwa dhumuni la uzinduzi wa vitabu hivyo ni kuongeza wigo wa ufahamu kwa wadau wote wa sekta ya kazi pamoja na jamii kwa ujumla, juu ya uwepo wa vitabu hivyo ambayo ni miongozo ya sheria katika kushughulikia na kutatua masuala mbalimbali katika sekta ya kazi ikiwemo migogoro inayotokana na mahusiano kazini.

Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Nalija Luhende akizungumza katika hafla hiyo ameipongeza Mahakama ya Tanzania, Divisheni ya Kazi kwa kazi nzuri inayofanya ya kutatua migogoro mbambali ya wananchi huku akimshukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kuialika OWMS kama mdau muhimu wa Mahakama kuhudhuria uzinduzi huu muhimu katika Sekta ya sheria nchini Tanzania.

Akizungumzia hatua mbalimbali zilizopigwa na Mahakama ya Tanzania hususani katika matumizi ya TEHAMA lakini pia katika maboresho mbalimbali Dkt. Luhende amesema kuwa mfano mzuri kwetu sisi ni matumizi ya mfumo wa TanzLII ambako maamuzi mbalimbali ya Mahakama yamekuwa yakiwekwa huko kwa wakati na kwa kufanya hivyo imetuwezesha sisi wadau wa Mahakama kupitia mfumo huu kujipatia kwa urahisi maamuzi mbalimbali ya Mahakama zote nchini Pamoja na nyaraka za sheria.

Akizungumzia kuhusu mambo yanayopelekea kuzalisha mashauri mbalimbali ya kazi Naibu Wakili Mkuu wa Serikali amesema kuwa ni wazi kuwa serikali ndio muajili mkubwa nchini hivyo jambo hili ndilo linalopelekea kuzalishwa kwa mashaurii ya kazi yanayotokana na hatua mbalimbali za kiutawala zinazochukuliwa na Serikali kama muajili, hatua hii inaifanya OWMS kama msimamizi wa Mashauri yote yanayofunguliwa dhidi ya Serikali kuwa mdau mkubwa sana wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.

“Uzinduzi wa Mkusanyiko wa mashauri ya kazi ni hatua muhimu sana kwetu sisi kama wadau wa Mahakama, tunatambua wazi kwamba mkusanyiko huu utasaidia kupunguza mashauri ambayo hayana tija pale ambapo kuna maamuzi ya Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani kuhusu mienendo ya mashauri ya kazi”. Alisema Dkt. Luhende.

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende ametoa wito kuwa, Pamoja na kuleta uelewa kwa wadau na taratibu mbalimbali za kimahakama tunatarajia kuwa mkusanyiko wa sheria hizi pia utaweza kupatikana kwa urahisi na ikiwezekana kwenye nakala laini (soft copy) ili kuwezesha wadau kuipata kwa urahisi Zaidi.

Akihitimisha hotuba hiyo Dkt. Luhende amemuomba mgeni rasmi Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kuwa Pamoja na kwamba OWMS inatambua jitihada za wazi zinazofanywa na Mahakama ya Rufani katika kumaliza Mashauri kwa wakati tunaomba kuwe na kikao maalum kuhusu Mashauri ya kazi (Special Session) ili kusaidia kupata maamuzi ya Mahakama ya Rufani ambayo yanatoa msimamo wa tafsiri ya sheria ambazo zinamaamuzi kinzani.

“Kama jambo hili litakupendeza Mhe. Mgeni Rasmi basi OWMS na wadau wengine tuko tayari kushirikiana na Mahakama kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa ili kuweza kupata suluhu na ufafanuzi muhimu wa Mahakama ya Rufani katika maamuzi yote kinzani” alisema Dkt. Luhende

Dkt.Luhende amemshukuru Mhe. Jaji Mkuu huku akiahidi kuwa OWMS itaendelea kudumisha uhusiano uliopo kati yake na Mahakama ili kusaidia upatikanaji wa haki kwa Serikali na kwa watanzania wote kwa ujumla.

Hafla ya uzinduzi wa Mkusanyiko wa Vitabu vya Mashauri ya Kazi, imehudhuriwa na maafisa mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania, akiwemo Kaimu Jaji Kiongozi, Mhe. John Mgetta na Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Temeke, maalumu kwa mashauri yanayohusu ndoa na talaka, Mhe. Ilvin Mugeta.

Wageni wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mkuu wa Shule ya Sheria, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Kazi (ILO-Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi), Bw. Wellington Chibebe, Majaji mbalimbali wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mawakili wa Serikali na wadau mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania.