Habari

Imewekwa: Oct, 04 2019

Fanyeni kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma

News Images

atumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wametakiwa kufanya kazi kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma, hatua itakayo wasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi.

Wito huo ulitolewa jana na Naibu Wakili Mkuu mpya wa Serikali Bwa. Gabriel Malata alipokuwa akiongea na watumishi hao, mara baada ya kutambulishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Clement Mashamba.

Akizungumzia umuhimu wa kufanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu za utumishi wa umma Bwa. Malata alisema kuwa hatua hiyo itatusaidiakuepukana na migogoro ya kiuhasibu inayoweza kujitokeza bila sababu yoyoye ya msingi.

“Ninawaomba sana watumishi wenzanu tushirikiane kufanya kazi kwa kufuata taratibu na sheria za utumishi wa umma ili huyu mtoto mchanga asijekuwa ndio kinara wa kuibua hoja za matumizi mabaya ya fedha za umma,” alisema Bwa. Malata.

Aidha Naibu Wakili Mkuu amesihi watumishi hao kufanya kazi kwa bidii huku akiwasisitizia zaidi watumishi wa kada ya sheria kujenga tabia ya kujisomea kwani kwa kufanya hivyo itawasaidia kuwa nguli katika fani hiyo.

Alisisitiza kuwa kama mwanasheria lazima ujue kuzungumza na Mahakama pamoja na kujua mahakama inataka nini wakati wote ili uyajue hayo yote ni lazima mawakili hao wawekeze katika kujisomea vitabu mbalimbali vinavyohusiana na masuala ya kisheria.

Naibu Wakili Mkuu aliwataka mawakili hao kujenga tabia ya kwenda mahakamani ili waweze kupata uzoefu wa kuendesha mashauri mbalimbali hatua itakayo wawezesha kuwa vinara katika uendeshaji wa mashauri tofautitofauti, badala ya kuwa na ujuzi wa kuendesha mashauri ya aina moja.

Aliongeza kuwa ni vyema kila mtumishi akatekeleza majukumu yake kwa ufasaha kwani kufanya kazi kwa bidii na kwa ukamilifu itawasaidia watumishi hao kujitangaza zaidi ndani na nje ya ofisi hiyo.

Bwa. Malata aliwaomba watumishi hao kuzingatia nidhamu wawapo kazini pamoja na kufika kazini mapema, ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kwa wakati.

Akizungumzia changamoto zilizopo, Naibu Wakili Mkuu wa Serikali amekili kuzifahamu changamoto hizo hivyo ameahidi kuzitafutia ufumbuzi wa haraka na kwa kuanzia amemshukuru MwanasheriaMkuu wa Serikali Dkt. Adelardus Kilangi kwa kumpatia sehemu ya vitabu vilivyokuwa vikitumiwa na ofisi yake ili viweze kutumiwa na Ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali wakati huu ambapo ofisi inajipamga kupata vitabu vingi zaidi.

Wakati huohuo Naibu Wakili Mkuu amewaasaa watumishi hao waachane na tabia za kusengenyana na kusemana badala yake wapendane na kuishi kama familia moja huku wakichapa kazi kwa bidii ili kwa pamoja waweza kulisukuma gurudumu la maendeleo mbele kwa manufaa ya taifa.

Naye Wakili Mkuu wa Serikali Dkt.Clement Mashamba akiongea wakati akimkaribisha Naibu Wakili Mkuu mpya, amesema mabadiliko haya yaliyofanywa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ni mabadiliko ya kawaida yenye lengo la kuiongezea nguvu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Dkt. Mashamba amewataka watumishi hao kumpa ushirikiano kiongozi huyo ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa urahisi na kwa ufanisi zaidi, wakati wote atakapokuwa akiwahitaji.

Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bwa. Gabriel Malata, amechukua nafasi ya Dkt. Ally Possi, ambaye aliteuliwa tarehe 20 septemba 2019 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli, kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kabla ya uteuzi huo Bwa. Malata alikuwa Kamishna wa kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu.