Habari

Imewekwa: Apr, 20 2024

Fanyeni kazi kwa kuzingatia Sheria zinazosimamia Utumishi wa Umma.

News Images

Watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria zinazosimamia Utumishi wa Umma, Haki na Wajibu wa Mtumishi wa Umma mahala a kazi ili waweze kufikia malengo yao kwa wakati.

Hayo yamesemwa leo terehe 18/04/2024 na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende wakati akifungua mafunzo kuhusu Haki na Wajibu wa Watumishi katika Utumishi wa Umma kwa Wajumbe wa Baraza la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Dkt. Luhende amesema kuwa Kupitia mafunzo hayo wajumbe watajifunza na kuzifahamu vyema Sheria zinazosimamia Utumishi wa Umma, Haki na Wajibu wa Mtumishi wa Umma itakayofundishwa na mkufunzi kutoka Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora sambamba na mada kuhusu Uendeshwaji wa Baraza la Wafanyakazi Mahala pa Kazi itakayotolewa na mkufunzi kutoka Ofisi ya Kamishna wa Kazi.

Ameongeza kuwa mada hizi mbili zimelenga kusaidia katika kuwajengea watumishi uwezo kuhusu masuala mbalimbali yanahusu Utumishi wa Umma hatua itakayosaidia watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi zaidi ikiwa ni amoja na kuondoa migongano inayoweza kujitokeza mahala pa kazi kati ya mtumishi na muajiri wake.

Amefafanua kuwa, Kupitia mada ya kwanza wajumbe hao watapata fursa ya kujifunza Sheria zinazosimamia Utumishi wa Umma, Haki na Wajibu wa Mtumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kujifunza kuhusu sheria taratibu na kanuni za utumishi wa Umma, katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Ameeleza kuwa kupitia mada hizi wajumbe hao watapata nafasi na wasaa mzuri wa kuuliza maswali ambayo yamekuwa yakiwatatiza kwa muda mrefu kuhusu masuala ya kupandishwa vyeo, maslahi ya watumishi na mambo mengine mengi ya kiutumishi ili kuweza kujibu maswali mbalimbali ambayo wamekuwa yakiulizwa kuhusu masuala ya utumishi wa Umma,

Amewasihi watumishi hao kutumia mafunzo hayo kupata uelewa kuhusu masuala ya kiutumishi ili waweze kufahamu wajibu walionao kwa Waajiri wao na kwa watanzania kwa ujumla kama watumishi wa umma hususani masuala mbalimbali ambayo mwajiri anatakiwa kuwafanyia au kuata kwa kuzingatia kuwa haki na wajibu ni vitu vinavyoenda pamoja.

kuhusu Uendeshwaji wa Baraza la Wafanyakazi Mahala pa Kazi Dkt. Luhende amesema kuwa mada hii itawasaidia wajumbe wa baraza kupata uelewa kuhusu maana ya baraza la wafanyakazi, sheria, kanuni na miongozo ya uundwaji wa baraza la wafanyakazi, muundo wa baraza la wafanyakazi, kazi za Baraza na umuhimu wa Baraza kwa taasisi za Serikali ikiwemo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Kuhusu uwepo wa dhana kuwa Baraza la wafanyakazi ni sehemu ya kupeleka malalamiko ya wafanyakazi Dkt. Luhende amefafanua kuwa dhana hii ni sahihi isipokuwa sio dhana kamili kuhusu uwepo wa Baraza la wafanyakazi kwa kuwa Baraza la wafanyakazi ndio chombo muhimu kwenye taasisi ambacho kikitumika ipasavyo kitasaidia kuleta mafanikio makubwa kwa taasisi husika.

Kiongozi huyo ameleza kuwa ni matarajio yake kwamba uelewa utakaopatikana kupitia mafunzo ya Baraza hili yatasaidia kuwaelimisha watumishi wengine ili kufanya Mkutano waBaraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuwa na tija katika utekelezaji wa majukumu yao kwa weledi zaidi na kwa wakati.

Naye Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Ndg. Mark Mulwambo Amesema kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa wajumbe ili kuweza kuwajengea uwezo na uelewa mbalimbali kuhusu Utumishi wa Umma na nafasi ya Mabaraza ya Wafanyakazi katika Ofisi za Umma ili yaweze kuwasaidia watumishi hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Akiwakumbusha umuhimu wa mafunzo haya Ndg. Mulwambo amesema kuwa mafunzo haya ambayo ni sehemu ya utangulizi wa Baraza la Wafanyakazi ni muendelezo wa kukidhi takwa la kisheria la kuwepo kwa Baraza la Wafanyakazi mahala pa kazi, ambapo OWMS imekuwa ikifanya vikao vyake vya Baraza mara mbili kila Mwaka.