Habari

Imewekwa: Oct, 22 2019

​Dkt Possi: Mafunzo kwa vitendo yapewe kipaombele kwa Watumishi

News Images

Dkt Possi: Mafunzo kwa vitendo yapewe kipaombele kwa Watumishi

Aliyekuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi, amewaomba viongozi wa Ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali kulipa kipaombele suala wa mafunzo kwa vitendo kwa watumishi wa ofisi hiyo hasa watumishi wa kada ya sheria ili waweze kutimiza majukumu yao kwa weledi.

Dkt. Possi ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa makabidhiano ya ofisi kati yake na Naibu Wakili Mkuu Mpya wa ofisi hiyo Bw. Gabriel Malata, mbele ya wajumbe wa menejimenti wakiongonzwa na Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Clement Mashamba.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Dkt. Possi amewashukuru wakurugenzi wa idara na vitengo pamoja watumishi wote wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano waliompa wakati wote wa uongozi wake kwani ushirikiano huo ndio ilikuwa chachu ya mafanikio yote yaliyopatikana wakati wa uongozi wake.

Akielezea mafanikio aliyoyapata Dkt. Possi amesema kuwa pamoja na mambo mengine kwa kushirikiana na Wakili Mkuu wa Serikali na watumishi wengine walifanikiwa kupata jengo la kudumu ambalo ndio linalotumiwa na ofisi hiyo sambamba na kuendesha mashauri mbalimbali hasa yale ya usuluhishi kwa kutumia mawakili wa serikali pekee.

Kuhusu mifumo ya Tehama Dkt. Possi amesema kuwa ni mhimu kuendeleza mifumo ya Tehama iliyopo kwa kuwa kupitia mifumo hiyo watumishi wataendelea kutimiza majukumu yao kwa urahisi huku akimuomba Makurungenzi wa Mashauri na Ubora Bw. Evarist Mashiba kushughulikia changamoto zilizopo katika mfumo wa Mashauri ili mfumo huo uweze kufanya kazi sanjari na kuongeza tija kwa watumishi wakati kutekeleza majukumu yao.

Dkt. Possi pia amewaomba watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kumpa ushirikiano Naibu Wakili Mkuu Mpya ikiwa ni pamoja na kuendeleza mahusiano mazuri yaliyokuwepo baina ya watumishi hao pamoja na taasisi nyingine za umma.

Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Gabriel Malata amemshukuru kiongozi huyo kwa kazi nzuri aliyoifanya hususani ya kutengeneza miundombinu mbalimbali katika ofisi hiyo huku akiahidi kuendeleza kazi nzuri aliyoianzisha kiongozi huyo.

Bw. Malata ameongeza kuwa katika utumishi wa umma hakuna kinachobadilika kwa kuwa utumishi wa umma ni ulele, hivyo mabadiliko yaliyofanyika ni mabadiliko yenye lengo la kuiongezea nguvu ofisi ya wakili Mkuu ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufasanisi zaidi.

“Nawashukuru kwa kazi kubwa mliyoifanya, nitaendelea kuienzi na niwahakikishie kuwa mtakuwepo kwenye vitabu vya kumbukumbu kuwa ninyi ndio waanzilishi wa ofisi hii. Alisema Bw. Malata.

Wakizungumza kwa niaba ya watumishi wa Ofisi hiyo Mhasibu Mkuu wa Ofisi hiyo Bi. Devota Ngulugulu na Mkurugenzi wa idara ya Madai Bw. Vincent Tangoh kwa pamoja wamemshukuru kiongozi huyo kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati wa uongozi wake na kumuahidi kumpa ushirikiano Naibu Wakili Mkuu mpya ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Bi. Ngulugulu amemuomba kiongozi huyo kuwa balozi mzuri wa ofisi hiyo popote atakapo kwenda hatua itakayosaidia kutangaza yale mambo mazuri yote yanayofanywa na ofisi hiyo.

Wakati huo huo Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Clement Mashamba amewasihi viongozi hao kuendelea kushilikiana ili kuweza kilisukuma mbele gurudumu la maendeleo mbele.

Amemuomba kiongozi huyo kutumia makongamano mbalimbali kila atakapopata nafasi ile aendelee kuitangaza ofisi hiyo pamoja na kazi zake ndani nanje ya nchi.

Mabadiliko ya uongozi katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yalitokea mnamo septemba 20 mwaka huu kufuatia uamzi uliofanywa na MhemiwaRais Dkt. John Pombe Magufuli wa kumteua aliyekuwa Naibu Wakili Mkuu huyo wa Serikali kuwa Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na nafasi yake kuchukukuliwa na Bw. Gabriel Malata aliyekuwa Kamishina wa Kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu.