Habari

Imewekwa: Jan, 19 2020

AG: Tumieni Mikutano ya Baraza la Wafanyakazi kuongeza ufanisi Kazini

News Images

Watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wametakiwa kutumia mikutano ya Baraza la wafanyakazi kujadili mambo yanayoleta tija kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa kazi miongoni mwao ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.

Wito huo umetolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi alipokuwa akizundua Baraza la Wafanyakazi wa ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali mapema leo katika mkutano uliofanyika ndani ya ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) uliopo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mkutano huo Prof. Kilangi amesema ili kufikia malengo ya nchi yetu ambayo ni pamoja na kuifanya Tanzania kufikia nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025, ni muhimu kuwa na uwazi katika ushirikishwaji baina ya viongozi wa taasisi mbalimbali za umma pamoja na watendaji ambao ni watumishi wa ngazi zote wanaozingatia Sheria, Taratibu na miongozo mbalimbali ya nchi.

“Naomba nitoe wito kwa wajumbe na washiriki wote wa Baraza hili kutumia fursa hii mliyoipata kuhoji na kutoa mapendekezo chanya yatakayokuwa na msaada kwa taasisi yenu ili hatimaye mchango wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali uonekane katika jitihada za pamoja katika kuiletea nchi yetu maendeleo.Alisema Pro. Kilangi.

Aidha Prof. Kilangi amempongeza Wakili Mkuu wa Serikali kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kwani kwa muda mfupi iliyoanzishwa wameweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kwa kuwatumia mawakili wa ndani ukilinganisha na fedha zilizotumika awali walipokuwa wanawatumia mawakili kutoka nje.

Akitolea mfano wa namna walivyoweza kuokoa fedha hizo Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema, kabla ya ofisi hii kuanzishwa katika shauri moja la nje ya nchi Serikali ingeweza kutumia mpaka shilingi bilioni 10 za Kitanzania tofauti na sasa ambapo serikali imekuwa ikitumia shilingi milioni 300 pekee.

Aliongeza kuwa usimamizi mzuri wa mashauri hayo umeisaidia Serikali kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho sasa kinatumika katika kujenga na kuimarisha miradi mikubwa ya kimaendeleo kama vile mradi wa Treni ya kisasa iendayo haraka (SGR) unaendelea kujengwa nchini.

Miradi mingine inayoendelea kujengwa kwa fedha za ndani ni mradi mkubwa wa umeme unaendelea kujengwa katika maporomoko ya mto Rufiji, (Nyerere Hydropower) madaraja makubwa, miradi ya Afya, Elimu pamoja na miundombinu ya barabara.

Vile vile ameipongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kuiwakilisha vyema Serikali katika Mahakama mbalimbali ndani na nje ya nchi katika kudai na kutetea haki za nchi kwa maslahi mapana ya Taifa letu.

Akizungumzia uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu, Prof. Kilangi ameitaka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kusimamia vyema mashauri yote ya uchaguzi yatakayo funguliwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Aliongeza kuwa pamoja na mambo mengine Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ndio yanye jukumu la kuisimamina kuiwakilisha Serikali Mahakamani katika kesi zote ninazohusiana na masuala ya uchaguzi hivyo nawasihi kuyasimamia vyema ili muweze kuwa sehemu ya kuivusha nchi yetu salama katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu.

Akielezea mafanikio yaliyofikiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo, Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Clement Mashamba amesema kuwa kwa kutumia mawakili wa Serikali katika kusimamia mashauri ya nje na ndani Serikali imeweza kuokoa takribani shilingi bilioni 1.5 fedha ambazo zimesaidia kuboresha miundombinu katika kuisaidia Tanzania kuelekea katika uchumi wa kati ifikapo 2025.

Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali amesema kuwa Ofisi yake itaendelea kusimamia kikamilifumajukumu yote yanayopaswa kusimamiwa na ofisi hiyo ili uwepo wa ofisi hiyo uweze kuleta tija katika kuhakikisha inatoa huduma bora ili kuweza kuisaidia nchi kufikia malengo yake iliyojiwekea.

Uzinduzi wa Baraza la wafanya kazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali umehudhuliwa pia na mwakilishi wa Kamishina wa Kazi Bi. Zevyanji Silungwe , Bi. Tabu Mambo katibu wa TUGHE mkoa wa Dar es Salaam, Wajumbe wa Menejiment ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na wajumbe wote wa Baraza la Wafanyakazi Tawi la Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.