Historia

Tarehe 13 Februari, 2018, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kwa Mamlaka aliyonayo chini ya Ibara ya36(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, alitoa “Amri ya Maboresho ya Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu” kupitia Tangazo la Serikali Na. 48 la mwaka 2018 kwa lengo la kuboresha huduma za kisheria katika sekta ya Umma.

Amri hiyo ya Maboresho ilitambua kuwepo kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yenye wajibu wa kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Idara za Serikali, na Mashirika ya Umma; kuandaaMiswaada ya Sheria; kuandaa nyaraka mbalimbali za Kisheria narasimu za Maazimio ya Bunge, n.k., sambamba na kuanzisha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inayoendesha mashtaka yote ya jinai mahakamani; na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inayosimamia na kuendesha mashauri yote yamadai na usuluhishi yanayoihusu Serikali.

Shughuli za Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zilihamishiwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mnamo mwaka 1965 hadi mwezi Februari mwaka 2018 ilipoanzishwa tena Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali. Hivyo, kutokana na maboresho hayo ya Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, mnamo tarehe 13 Februari, 2018, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliona umuhimu wa kuirudisha tena Ofisi hiyo, ambapo alitoa Amri ya Kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kupitia Tangazo la Serikali Na. 50 la 2018.

Tarehe 15 Aprili 2018, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua Dkt. Clement Julius Mashamba kuwa Wakili Mkuu wa Serikali na Dkt. Ally Saleh Possi kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali. Aidha, tarehe 7 Julai 2018, Mhe. Rais wa Jamhuri wa Mungano wa Tanzania aliidhinisha Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.