Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

TAASISI ZATAKIWA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO ILI KUEPUSHA MIGOGORO

Imewekwa: 26 September, 2026
TAASISI ZATAKIWA KUSHUGHULIKIA MALALAMIKO ILI KUEPUSHA MIGOGORO

Taasisi za umma na mashirika nchini zimetakiwa kuhakikisha zinashughulikia malalamiko yanayojitokeza katika maeneo yao ili kuepusha migogoro ikiwemo ya kibiashara.

Akizungumza jijini Dar-es-salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Usuluhishi wa Ndani kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) Wakili David Kakwaya amesema kuwa taasisi za Serikali zinatakiwa kushughulikia malalamiko mbalimbali yanajitokeza kwa wakati ili kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza katika maeneo yao.

Hayo ameyazungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Wakili House jijini Dar es Salaam wakati wa kutambulisha ujio wa Wiki ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara Tanzania na mkutano wa Kilele cha Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara utakaofanyika jijini Dar-es- salaam kuanzia tarehe 28 Septemba, 2026 hadi tarehe 02 Oktoba 2026. OWMS itatoa wakufunzi na kushiriki kwenye Wiki hiyo ambapo mafunzo na kongamano kuhusu usuluhishi wa migogoro ya kibiashara yatatolewa.

“Usiposhughulikia malalamiko yatazalisha migogoro kwa hiyo Ofisi yetu imekuwa ikitoa elimu kwa taasisi za umma namna ya kushughulikia malalamiko ya wakandarasi na wafanyabiashara mbali mbali kabla malalamiko hayo hayajafikia hatua ya kuwa migogoro kwa kuwa ukiyashughulikia malalamiko mapema unapunguza na kuzuia migogoro kwa kiasi kikubwa kwa kuwa ushughulikiaji wa migogoro unahusisha matumizi ya fedha na upotevu wa muda,” amesema Wakili Kakwaya.

Nae Wakili Mpale Mpoki akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi Tanzania (TIAC) ameongeza kuwa Wiki hiyo itawakutanisha watunga sera, wafanyabiashara, washirika wa maendeleo,

wataalam wa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR) na wadau wengine ambapo sehemu ya mafunzo itawapa washiriki fursa ya kuongeza ujuzi na maarifa ya vitendo katika ADR na utatuzi wa migogoro ya kibiashara. Kliniki ya ADR na shughuli za uhamasishaji kwa umma zitatoa fursa ya kuwafikia na kuwashirikisha wananchi na wadau.

Aidha, Wakili Mpoki aliongeza kuwa malengo  ya mafunzo na  kongamano hilo ni kuongeza uelewa wa mifumo ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR), kuimarisha  uwezo na ujuzi wa kitaalamu wa wadau wanaohusika katika utatuzi wa migogoro ya kibiashara, kujenga na kuimarisha imani katika usuluhishi, upatanishi na  mifumo mengine ya ADR, kukuza majadiliano kuhusu namna ya kuongeza ufanisi na upatikanaji wa huduma za utatuzi wa migogoro ya kibiashara, kuchunguza ubunifu na matumizi sahihi ya teknolojia katika ADR, kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, wataalam wa sheria, sekta ya biashara, taasisi za elimu na wadau wengine na kuchangia katika kuendeleza na kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro ya biashara nchini Tanzania.

Wiki hiyo imebebwa na kauli mbiu isemayo, “Kujenga Imani Katika Utatuzi wa Migogoro kwa Njia  Mbadala  (ADR): Kuimarisha  Ufanisi, Upatikanaji na Ubunifu  katika Utatuzi wa  Migogoro ya Kibiashara.”

Mafunzo na kongamano hilo limeandaliwa na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi Tanzania (TIAC) kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria (MoCLA), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (OAG), Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) na Shule ya Sheria Tanzania (LST).