Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA NJIA MBADALA YA USULUHISHI (ADR) KUPUNGUZA GHARAMA ZA MIGOGORO YA BIASHARA

Imewekwa: 02 October, 2026
SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA NJIA MBADALA YA USULUHISHI (ADR) KUPUNGUZA GHARAMA ZA MIGOGORO YA BIASHARA

Serikali imesisitiza umuhimu wa kutumia Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala (ADR) katika migogoro ya kibiashara ikielezwa kuwa njia hiyo inaweza kusaidia kupunguza muda na gharama za migogoro na kuimarisha imani ya wawekezaji na wafanyabiashara katika mazingira ya biashara nchini.

Kauli hiyo imetolewa kwenye ufunguzi wa kongamano la Wiki ya Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara Tanzania na Mkutano wa Kilele wa Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara 2026 iliyoandaliwa na Kituo cha Kimataifa cha Usuluhishi Tanzania (TIAC) kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali na Shule ya Sheria Tanzania (LST).

Akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Zainab Katimba (Mb), Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice E. Mtulo amesema matumizi ya ADR ni muhimu katika kutatua migogoro kwa ufanisi kwa kuzingatia umuhimu wa biashara na uwekezaji katika maendeleo ya nchi.

“Tunapozungumzia utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, tunahitaji ushirikiano wa wadau wote. Wizara ya Katiba na Sheria ina nafasi muhimu katika kuweka mazingira mazuri ya kisheria, kitaasisi na kiutendaji,” amesema Bi. Mtulo.

Bi. Mtulo aliongeza kuwa Serikali, mahakama, wanasheria, wasuluhishi na wasomi wana nafasi muhimu katika kuhakikisha mifumo ya ADR inaendelea kuimarishwa ambapo alisisitiza umuhimu wa kuzingatia uadilifu, uhuru na imani ya umma katika mchakato wa utatuzi wa migogoro.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TIAC, Wakili Godson Nyange, amesema wiki hiyo imeandaliwa kwa lengo la kuwaunganisha wadau mbalimbali wa utatuzi wa migogoro ya kibiashara na kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya njia mbadala badala ya kutegemea mifumo ya kawaida ya kimahakama pekee.

Nyange alisema migogoro ya kibiashara inaweza kuanzia katika biashara ndogo, kati, kubwa hadi biashara za kimataifa ambapo alibainisha kuwa mikataba isiyoandaliwa kwa ufasaha na uelewa wa kutosha inaweza kuwa chanzo cha migogoro.

“Kuna hatua tatu. Kwanza hatua ya mikataba ili kuzuia migogoro isitokee, hatua ya pili ni pale ambapo migogoro imeshatokea. Tunakwenda mahakamani na kwenye mabaraza ya usuluhishi. Hapo sasa ndipo kituo kinapokuwa na umuhimu zaidi kwa sababu faida za utatuzi mbadala wa migogoro zinafahamika, zinapunguza muda na gharama,” alisisitiza Wakili Nyange.

Naye Mkurugenzi wa Sehemu ya Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala (ADR), Felix Chakila wa Wizara ya Katiba na Sheria amesema Serikali inaendelea kuweka mifumo na taratibu zinazolenga kujenga imani kwa wawekezaji wa ndani na nje, pamoja na wafanyabiashara ili kuhakikisha migogoro inapojitokeza inapata utatuzi unaofaa.

 Chakila alisema matumizi ya ADR yanaweza kusaidia kuokoa fedha ambazo zingeweza kutumika katika taratibu za kawaida za kimahakama na kusaidia wahusika wa mgogoro kufikia suluhu kwa namna inayowezesha kuendelea kwa mahusiano yao.

Wiki hiyo imejikita katika kaulimbiu isemayo, “Kujenga Imani katika Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala (ADR): Kuimarisha Ufanisi, Upatikanaji na Ubunifu katika Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara,” ikiwa na lengo la kuongeza uelewa na matumizi ya ADR katika sekta ya biashara na uwekezaji nchini.