Habari

Imewekwa: Mar, 09 2024

SERIKALI YASHINDA SHAURI LA USULUHISHI KATIKA BARAZA LA KIMATAIFA LA BIASHARA (ICC)

News Images

Tarehe 06 Machi, 2024, Baraza la Kimataifa la Biashara (International Chamber of Commerce-ICC) limetoa uamuzi wake na kuipa Serikali ushindi katika Shauri la Usuluhishi Na. 2682/AZO baina ya Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency-PBPA) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Kampuni ya Alchemist Energy Trading DMCC kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu.

Shauri hili lilifunguliwa baada ya Kampuni ya Alchemist Energy Trading DMCC kushindwa kusambaza mafuta kwa mujibu wa Mkataba ulitokana na Zabuni Na. PBPA/CPP/PMC/C3-KOJI/02/2021 wa tarehe 05 Januari 2021 kwa ajili ya kuleta nchini mafuta Metriki za Ujazo 36,192 ambayo yalipaswa kupokelewa kuanzia tarehe 27 Februari, 2021 hadi tarehe 01 Machi, 2021.

Kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jopo la utetezi liliongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende akishirikiana na Mawakili wengine kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

Katika uamuzi wake, Baraza la ICC limetamka kuwa Kampuni ya Alchemist Energy Trading DMCC ilivunja Mkataba na hivyo kuwaamuru kurejesha fedha kwa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) dola za Marekani milioni tisa, laki saba na kumi elfu, mia sita hamsini na moja na senti arobaini na tano (USD 9,710,651.45) pamoja na riba kabla ya tuzo (pre-award interest) asilimia 7.67% kuanzia tarehe 18 Mei, 2021 hadi Novemba, 2023; kwa kuvunja Mkataba na kushindwa kuleta mafuta nchini.


Pamoja na Kampuni ya Alchemist Energy Trading DMCC kuamuriwa na Baraza hilo kurejesha fedha tajwa hapo juu kwa kuvunja Mkataba, pia Kampuni hiyo inatakiwa kutekeleza yafuatayo:-

  • (i)Kuilipa PBPA dola za Marekani milioni moja, laki moja arobaini elfu, na arobaini na nane (USD 1,140,048.00) ikiwa ni adhabu ya kuharibu mfumo wa ununuzi wa mafuta wa pamoja;
  • (ii) Kuilipa PBPA dola za Marekani laki nane themanini na mbili elfu (USD 882,000.00) ikiwa ni gharama za Baraza;
  • (iii)Kuilipa PBPA shilingi milioni mia nane kumi na nane elfu, laki mbili themanini na tano na mia saba (TZS 818,285,700.00) ikiwa ni gharama za kesi; na
  • (iv)Kulipa riba baada ya tuzo (post award interest) asilimia 7.67% kuanzia tarehe 06 Machi, 2024 hadi atakapokamilisha malipo yote anayodaiwa.

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inatoa shukrani za dhati kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, PBPA na wadau wote walioshiriki katika kuendesha shauri hili la kimataifa kwa kutumia Mawakili wa Serikali wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali itaendelea kusimamia na kuendesha mashauri ya kimataifa kwa weledi na kulinda maslahi mapana ya Taifa letu.