Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

OWMS KIELELEZO CHA UZALENDO KATIKA KULINDA RASILIMALI ZA TAIFA

Imewekwa: 28 November, 2026
OWMS KIELELEZO CHA UZALENDO KATIKA KULINDA RASILIMALI ZA TAIFA

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) mepongezwa kwa uendeshaji wa mashauri ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake ndani na nje ya nchi.

 

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Baraka Luvanda wakati anafungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali uliofanyika jijini Dodoma.

 

 Mhe. Luvanda ameipongeza OWMS kwa uendeshaji wa mashauri na ari ya kujituma ambapo ni kielelezo cha uzalendo uliotukuka katika kulinda rasilimali za taifa. Serikali inatambua mchango wenu hivyo niwatie shime katika kuendelea kuendesha mashauri kwa niaba ya Serikali.

 

 “Niwapongeze kwa kuokoa fedha ambazo Serikali ingepaswa kulipa endapo tungeshindwa mashauri hayo,” amesema Mhe. Balozi Luvanda. Pia, ameongeza kuwa Baraza ni jukwaa muhimu linalounganisha menejimenti na wafanyakazi ambapo watumishi wanapata nafasi ya kutoa maoni yenye tija ya kuboresha utendaji kazi na alitoa rai kwa wajumbe kutumia nafasi hiyo kutoa maoni na kuwa na maazimio yatakayoboresha utendaji kazi wa Ofisi wenye ufanisi kwa maslahi ya taifa.

 

 Akiwasilisha taarifa kwa wajumbe wa Baraza hilo, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Julai, 2026 hadi Disemba, 2026; OWMS imeendesha jumla ya mashauri mapya 3,069, kuhitimisha mashauri 1,116 ya madai na kuokoa takribani shilingi bilioni 432.83 ambazo ni sawa na kutengeneza takribani kilomita 200 za barabara ya lami.

 

 Dkt. Possi aliongeza kuwa katika  kipindi hicho, OWMS imeendesha mashauri ya usuluhishi 292 ambapo kati ya hayo mashauri 81 ni mapya, imehitimisha mashauri 34 yakiwemo mashauri 32 ya kitaifa na mashauri mawili (02) ya kimataifa na kuokoa shilingi bilioni 25.92 na dola za Marekani milioni 420 (ambazo ni sawa na shilingi trilioni 1.25) ambazo Serikali ingelazimika kulipa endapo tungeshindwa mashauri hayo.

 

“Dola za Marekani milioni 420 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 1.25 zilizookolewa zinatosha kujenga hospitali 12 za kisasa za ngazi ya mkoa na vifaa vyake,” amefafanua Dkt. Ally Possi.

 Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice E. Mtulo amesema kuwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wamepatiwa mafunzo kuhusu fidia kwa wafanyakazi na Meneja wa Kanda ya Kati wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Bi. Nuru Ashraf na mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya akili unde yaliyotolewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Mahadia Tunga.

 

 Bi. Mtulo amesema kuwa mafunzo hayo yataongeza uelewa kwa wafanyakazi kuhusu masuala ya fidia kwa wafanyazi na yatapanua wigo wa matumizi ya TEHAMA mahali pa kazi ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu kwa haraka na kwa wakati kwa kuzingatia matumizi sahihi ya akili unde.

 

 “Nitoe rai kwa Mawakili na watumishi wa OWMS kuzingatia matumizi sahihi ya akili unde kwa kuwa Ofisi hii inafanyia kazi nyaraka nyeti na muhimu za Serikali zinazohitaji usiri,” amesisitiza Bi. Mtulo.

 

 Bi. Mtulo amesema kuwa mkutano wa Baraza hufanyika mara mbili kwa mwaka ambapo uwepo wa Baraza hilo ni dhamira ya Serikali ya ushirikishwaji wa wafanyakazi mahali pa kazi ili kuimarisha ushirikiano kati ya menejimenti na wafanyakazi katika utekelezaji wa majukumu, ustawi na maendeleo ya taasisi.