Habari

Imewekwa: Apr, 20 2024

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yatakiwa Kuendelea kutumia Baraza la Wafanyakazi kuimarisha Ushirikishwaji.

News Images

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imetakiwa kutumia Baraza la Wafanyakazi hatua itakayosaidia kuimarisha ushirikishwaji ili watumishi waweze kufanya kazi kwa kuzingatia rasilimali zilizopo kufikia malengo waliyojiwekea kwa wakati.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa niaba ya Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana uliofanyika mkoani Morogoro.

Mhe. Sagini amesema kuwa watumishi wanaposhirikishwa masuala yanayowahusu kupitia vikao mbalimbali kama hivi vya Baraza la wafanyakazi inasaidia kwa kiasi kikubwa kupanga mipango madhubuti ambayo kwa kiasi kikubwa inasaidia taasisi za Serikali kupiga hatua katika kuhakikisha inafikia malengo yake kwa wakati.

Kiongozi huyo amesema kuwa Baraza hili ni jukwaa muhimu sana mahala pa kazi kwani ni kiunganishi kati ya Menejimenti na Wafanyakazi, ndio maana ni muhimu Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuendelea kuwashirikisha watumishi wake ili kuleta ufanisi kwa Mamlaka na Taifa zima kwa ujumla.

Mhe. Sagini ametumia Mkutano huo kuwakumbusha watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuwa Serikali inazingatia sana suala la taasisi zake kuwa na Mabaraza ya Wafanyakazi kwani yalianzishwa kisheria kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi za Idara, Taasisi na Wizara kuhusu usimamizi wa kazi na rasilimali watu, utekelezaji wa majukumu, kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora za kazi, maslahi ya watumishi na kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi.

Aidha, Mhe. Sagini ameongeza kuwa wajibu wa mabaraza haya ni kuwa vyombo vya ushauri na usimamizi katika kuhakikisha kuwa waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao, pia wanazingatia maadili ya utumishi wao ili kuleta matokeo ya utendaji wa kazi yenye tija katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Naibu Waziri amepongeza Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kufanikisha Baraza la Wafanyakazi kwa kuwa matunda ya uwepo wa Baraza la Wafanyakazi yameanza kuonekana.

Akiyataja mafanikio hayo kiongozi huyo amebainisha kuwa mafanikio hayo ni pamoja na kuwashirikisha wafanyakazi katika maamuzi mbalimbali ikiwemo kuwasilisha changamoto mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi, kama ambavyo ilivyo sasa moja kati ya madhumuni ya mkutano huu ni kuwawezesha wafanyakazi kupitia makadirio ya Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/2025 kwa kuzingatia ukomo wa Bajeti, malengo ya Taasisi na maeneo ya vipaumbele.

Amefafanua kuwa utaratibu wa kuwepo kwa Baraza la Wafanyakazi unalenga kukuza uwazi na ushirikishwaji katika maamuzi mbalimbali ya Mamlaka ili mtumishi anapotekeleza majukumu yake awe akifahamu Dira na Dhima ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali zinamtaka afanye nini, ikiwa ni pamoja na mtumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali anapaswa kufahamu bajeti iliyotengwa kwa ajili ya shughuli zake ndani ya Taasisi ili afanye kazi kwa kuzingatia malengo na rasilimali zilizokadiriwa kutumika.

Ametumia mkutano huo kuwakumbusha watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kwa dhati kuondoa uzembe na vitendo vyote vya rushwa mahala pa kazi, hii ni pamoja na kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza tija, katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Ameongeza kuwa ni wajibu wa kila mtumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu Serikali kuhakikisha anafahamu wajibu wake mahali pa kazi, ili aweze kutekeleza majukumu aliyopangiwa na kuhakikisha anayakamilisha katika muda uliopangwa, hali kadhalika ahakikishe anatunza mali na vifaa alivyokabidhiwa kufanyia kazi. Bila kusahau wajibu wa kuwahi kazini, kufanya kazi kwa bidii na kuwa na uzalendo kwa taifa wakati wa utekelezaji wa majukumu yake.

Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende, amesema kuwa Uwepo wa Baraza la Wafanyakazi ndani ya OWMS umekuwa na manufaa makubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi hii kwa kuwa Baraza la wafanyakazi limeamsha ari ya uchapakazi kwa watumishi na kuboresha ushirikishwaji wa Wafanyakazi katika majukumu ya kila siku ya Ofisi hii, hivyo kupelekea mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka sita tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.

Akizungumzia kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika uendeshaji wa mashauri Dkt. Luhende amesema kuwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Aprili 2024 Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imeendesha kwa mafanikio makubwa mashauri 7992 ambapo kati ya hayo mashauri ya madai yalikuwa 7813 na 179 ya usuluhishi.

Ameongeza kuwa Katika kuendesha mashauri 7813 ya madai, mashauri 762 yalimalizika. Aidha, kati ya mashauri ya madai yaliyomalizika, mashauri 719 yalihitimishwa kwa njia ya kimahakama na mashauri 43 yalihitimishwa kwa njia ya majadiliano nje ya mahakama.

Ameeleza kuwa Katika kuendesha mashauri 7813 ya madai, mashauri 762 yalimalizika. Aidha, kati ya mashauri ya madai yaliyomalizika, mashauri 719 yalihitimishwa kwa njia ya kimahakama na mashauri 43 yalihitimishwa kwa njia ya majadiliano nje ya mahakama.

Kwa kipindi tajwa, OWMS ilishinda jumla ya mashauri 705 na kufanikiwa kuokoa fedha za Serikali jumla ya Shilingi Trilioni 3.47 ambazo zingelipwa iwapo serikali ingeshindwa mashauri hayo pia Ofisi imeokoa jumla ya Shilingi Bilioni 10.2 zilizotokana na mashauri 43 yaliyohitimishwa kwa njia ya majadiliano nje ya Mahakama na kufanya jumla ya kiasi kilichookolewa kufikia Shilingi Trilioni 3.48.

Ameyataja Mafanikio mengine yaliyotokana na uwepo wa Baraza la Wafanyakazi kuwa ni watumishi wa OWMS kushirikishwa moja kwa moja katika majukumu mbalimbali ya kitaasisi, kupitia uandaaji wa nyaraka kama vile Bajeti ya kila mwaka, Mpango kazi wa kila mwaka na Mpango Mkakati wa OWMS wa Miaka Mitano (2021/2026).

Aidha, watumishi wamepata nafasi za kuwasilisha mapendekezo, changamoto mbalimbali katika utendaji kazi wa Ofisi, na kuzitafutia ufumbuzi, kupitia vikao vya idara na Vitengo, vikao vya wafanyakazi wote pamoja na vikao vingine vya kisheria kama Baraza la wafanyakazi.

Naye Kaimu Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Ndg. Mark Mulwambo amesema kuwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali itaendelea kuwashirikisha wafanyakazi katika kutoa maoni ikiwemo kupokea changamoto zitakazowasilishwa na watumishi ili kuzitafutia ufumbuzi kupitia vikao vya idara, vikao vya wafanyakazi wote pamoja na vikao vingine vya kisheria kama Baraza la wafanyakazi ili kuboresha utendaji na ufanisi wa utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kama ilivyo sasa pamoja na mambo mengine, madhumuni ya mkutano huu ni kuwawezesha wafanyakazi kupitia Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu masuala ya Bajeti ya OWMS.

Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ulitanguliwa na Mafunzo kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi na kufunguliwa na Wakili Mkuu wa Serikali ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza, Mhe. Dkt.Boniphace Luhende, ambapo kupitia mafunzo hayo, wajumbe walifundishwa mada kuhusu Sheria zinazosimamia Utumishi wa Umma, Haki na Wajibu wa Mtumishi wa Umma mada iliyowasilishwa na Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na mada kuhusu Uendeshwaji wa Baraza la Wafanyakazi Mahala pa Kazi mada hii iliwasilishwa na Ofisi ya Kamishna wa Kazi.