Habari

Imewekwa: May, 22 2024

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini amewataka Mawakili wa Serikali kutoa ushauri mapema.

News Images

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini amewataka Mawakili wa Serikali kutoa ushauri mapema kabla mambo hayajaharibika. Ni vema mtoe ushauri mapema pale ambapo mnaona jambo lina dalili ya kuharibika kwa kushauri vema viongozi wa taasisi zao ili kuiepusha Serikali na taasisi zake kuzalisha mashauri na migogoro mbali mbali nchini.

Hayo yameelezwa na Mhe. Sagini wakati akifungua mafunzo kwa Mawakili wa Serikali zaidi ya mia tano yaliyopangwa kufanyika kwa siku tatu jijini Arusha kuanzia tarehe 20 Mei, 2024. Pia, alizindua nembo ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo imechapishwa kwenye Gazeti la Serikali Toleo Na. 19 la tarehe 10 Mei, 2024 na iko tayari kuanza kutumika. Mhe. Sagini alifungua mafunzo hayo na kuzindua nembo hiyo kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Dkt. Balozi Pindi Chana.

Aliongeza kuwa matarajio ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mawakili wa Serikali baada ya kupata mafunzo hayo ni kuwa chachu katika usimamizi na utatuzi wa migogoro ya mikataba inayotokana na Sekta ya Ujenzi kwani nchi yetu ipo kwenye ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati; kuwa chachu katika kupunguza na kutatua migogoro ya uwekezaji katika Sekta ya Madini na rasilimali za nchi; kupunguza idadi ya mashauri ya madai na usuluhishi yanayofunguliwa na yanayoendelea kwa kuyamaliza kwa njia ya usuluhishi hivyo kuimarisha juhudi za Serikali katika kuvutia wawekezaji na kutekeleza miradi mbali mbali nchini; kuwashauri waajiri ipasavyo kuhusiana na taratibu za uendeshaji wa mashauri ya nidhamu pale wanapohitajika kuchukua hatua za nidhamu dhidi ya watumishi wa umma; kuishauri ipasavyo Serikali na taasisi zake wakiwemo viongozi wa ngazi mbalimbali kuhusu namna bora ya kumaliza migogoro na wananchi au wawekezaji bila kuathiri maslahi ya nchi; na kusimamia na kuendesha vizuri mashauri ya uchaguzi yatakayofunguliwa kabla na baada ya uchaguzi mkuu pamoja na uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Akizungumza wakati wa akimkaribisha Mgeni Rasmi Mhe. Sagini, Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuendelea kuwanoa Mawakili wa Serikaliili kuboresha utendaji kazi wao; kupunguza ongezeko la mashauri kwenye baadhi ya maeneo yanayozalisha migogoro mingi dhidi ya Serikali ambapo hadi kufikia Mwezi Aprili, 2024 Ofisi imeendesha jumla ya mashauri 7,813 na kati ya hayo mashauri ya ndani ni 7,798 na mashauri ya nje ya nchi ni 15 na kati ya mashauri hayo, mengi yametokana na migogoro ya ardhi, kazi, mikataba, manunuzi, bima, Katiba na haki za binadamu.

Aidha, Ofisi imeendesha jumla ya mashauri ya usuluhishi 179 na kati ya hayo mashauri 148 ni ya ndani ya nchi na mashauri 31 ni ya nje ya nchi na mengi yametokana na mikataba ya ujenzi, uwekezaji na taratibu za manunuzi. Vile vile, Ofisi imeshughulikia notisi za siku 90 zipatazo 723 zilizowasilishwa katika kipindi cha mwezi Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 na asilimia kubwa ya notisi hizo zinahusu masuala ya ardhi, kazi na mikataba ambayo taasisi za Serikali zimeingia na wadau mbalimbali.

Pia, Dkt. Luhende aliongeza kuwa tangu Ofisi imeanza kufanya mafunzo hayo wameshuhudia ongezeko la ubora wa kazi zinazotekelezwa na imeiwezesha Ofisi kuwa na mafanikio mbali mbali ikiwemo Serikali kushinda mashauri ya madai 743 yenye thamani ya shilingi bilioni 406.4 na mashauri 15 ya usuluhishi yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.5.

Aidha, Ofisi imeendesha na kushinda mashauri yenye umuhimu mkubwa kwa ustawi wa taifa letu ambayo ni shauri la ujenzi wa mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima-Uganda mpaka Chongoleani – Tanga ambapo Serikali ingeshindwa mradi huu wenye takribani shilingi trilioni 8 usingeweza kutekelezwa; mkataba wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaamna uwekezaji wa kiwanda cha saruji Tanga na iwapo Serikali ingeshindwa uwekezaji huo usingeweza kufanyika; na kushinda shauri la usuluhishi la kimataifa lenye lenye takriban shilingi bilioni 36 baina ya Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya kampuni ya Alchemist Energy Trading DMCC kupitia uamuzi wa Baraza la Kimataifa la Biashara (ICC).

Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo alisema kuwa mafunzo hayo ni muendelezo wa mipango ya Ofisi hiyo ya kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali wa Ofisi hiyo na waliopewa hati idhini ya kuendesha mashauri kwa niaba ya Ofisi hiyo. Amefafanua kuwa mafunzo hayo yanajumuisha washiriki kutoka kwenye Wizara, taasisi, mashirika ya umma, mamlaka za Serikali za Mitaa, tume, vyuo vikuu, mabenki na bodi mbali mbali pamoja na washiriki kutoka Zanzibar.

Aidha, ameongeza kuwa mafunzo hayo yatatolewa na wakufunzi kumi na moja wabobezi ambao ni Majaji na Majaji wastaafu kutoka Mahakama Kuu ya Tanzania, wanataaluma na wataalam wabobezi wa Sekta ya Sheria nchini, wakufunzi kutoka vyuo vikuu nchini na wataalamu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.