Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali

MICHEZO YA SHIMIWI YAFUNGULIWA, ZAWADI KWA WASHINDI KUBORESHWA

Imewekwa: 29 September, 2026
MICHEZO YA SHIMIWI YAFUNGULIWA, ZAWADI KWA WASHINDI KUBORESHWA

Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ya 40 kwa mwaka 2026 imefunguliwa rasmi tarehe 26 Septemba 2026 katika viwanja vya Chuo cha Mafunzo ya Polisi (CCP) Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Ufunguzi rasmi wa mashindano ya SHIMIWI umefanywa na mgeni rasmi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda (Mb) na kumehudhuriwa na watumishi kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Makonda ameipongeza Kamati Tendaji ya SHIMIWI kwa kuhakikisha michezo hiyo inaendelea kufanyika kila mwaka na alisisitiza umuhimu wa kufanya maboresho zaidi katika michezo hiyo.

Mhe. Makonda ameomba kuwa michezo hiyo kwa mwaka 2027 ifanyike mkoani Arusha huku akiahidi kufanya mapinduzi na mabadiliko makubwa wakati wa maandalizi hususan eneo la zawadi kwa washindi ikiwemo uwepo wa zawadi mbalimbali ikiwemo fedha taslimu.

Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Makonda alisema michezo si afya tu, michezo si uchumi tu, bali ni umoja wetu na ushirikiano wetu ambao umekuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha watumishi wanatekeleza majukumu yao kwa wakati.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya SHIMIWI, ndugu Daniel Mwalusamba akitoa salamu za Kamati pamoja na wanamichezo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali na kuruhusu michezo hiyo kufanyika ikiwa ni pamoja na kuwawezesha watumishi kushiriki kikamilifu.

Pia, Mwalusamba ameahidi kusimamia michezo hiyo kwa ufanisi na kuhakikisha watumishi waliofika mkoani Kilimanjaro wanashiriki ipasavyo na wanazingatia kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Naye, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS), Bi. Asha Hayeshi amesema ushiriki wa OWMS katika mashindano ya SHIMIWI utasaidia watumishi kuimarisha afya zao kupitia michezo ili kuwa na afya njema ya kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao kwa wakati na kwa ufanisi zaidi.

Bi. Hayeshi aliongeza kuwa michezo ni sehemu muhimu ya ustawi wa watumishi kwa kuwa inaimarisha afya ya mwili na akili na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. Hivyo, kuwawezesha watumishi kuwa na ari na nguvu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Aidha, Bi. Hayeshi alisema ushiriki wa OWMS katika mashindano hayo utatoa fursa kwa watumishi kuimarisha mahusiano na kujenga ushirikiano mzuri baina yao na watumishi kutoka taasisi nyingine za Serikali hatua itakayowaongezea maelewano na kubadilishana uzoefu ili kutekeleza majukumu ya Serikali kwa ufanisi.

 

Michezo ya SHIMIWI kwa mwaka 2026 inafanyika kitaifa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki mashindano hayo kwa lengo la kuhakikisha michezo hiyo inawawezesha watumishi wa Serikali kukutana, kushirikiana na kujenga mahusiano mema, kuimarisha afya, utimamu wa mwili na akili. ‎

Michezo ya SHIMIWI ya mwaka 2026 inaongozwa na kaulimbiu isemayo “Watumishi Wa Umma Tupo Tayari Kwa Afcon 2027".