Habari

Imewekwa: Jan, 24 2022

Mheshimiwa Jaji Mkuu azindua Juzuu za taarifa ya Sheria.

News Images

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, mapema leo amezindua Juzuu ya Taarifa ya Sheria za Tanzania kutoka Mwaka 2007 hadi 2020 zinazo yojumuisha maamuzi ya Mahakama Kuu Tanzania Bara na Visiwani pamoja na Mahakama ya Rufani.

Uzunduzi wa Juzuu hizo umenda pamoja na uzinduzi wa Faharisi (Index) ya Sheria Mama na Sheria ndogo za kuanzia Mwaka 1961 mpaka mwaka 2020, vyote vikiwa katika mfumo wa nakala laini na ngumu, hatua ambayo imelenga kuwasaidia maafisa wa Mahakama na Wadau kutumia vitabu hivyo vya sheria katika kusimamia utoaji haki nchini.

Sambamba na tukio hilo Mhe. Jaji Mkuu amezindua mfumo mpya wa kielektroniki kwa ajili ya kusajili, kutunza kumbukumbu na kuratibu leseni za Mawakili, (e-Wakili Management System) mara baada ya mfumo uliokuwa unatumika awali kuwa na changamoto kadhaa zilizopelekea zoezi hilo kutofanyika kwa ufanisi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Jaji Mkuu Prof. Juma amesema kuwa hii ni mara ya tatu kwa machapisho hayo kutolewa na Mahakama ya Tanzania ambapo Chapisho la kwanza lilikuwa kati mwaka 1980 hadi 1996 huku Chapisho la pili lilikuwa kati ya mwaka 1997 hadi 2006. Amesema kuwa uamuzi wa mashauri mengi katika Chapisho la tatu utaonekana kuwa ni wa Mahakama ya Rufani ikiwa ni muendelezo wa kutoa nakala nyingine za uamuzi wa Mahakama Kuu Tanzania bara na Visiwani kwa kila mwaka husika kuwa na chapisho la pili.

Prof. Juma alieleza kuwa machapisho ya mwanzo kabla ya uhuru yalianza Mwaka 1921 wakati Mahakama Kuu ya Tanganyika inaanza shughuli zake tarehe 3 Januari, 1921 ambapo maamuzi katika mashauri mengi kwa kipindi hicho yalitolewa taarifa kati ya mwaka 1921 mpaka 1952 ambayo yaliitwa (Tanganyika Territory Law Reports), hii ikiwa ni chapisho la kwanza.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu Prof. Ibrahimu Hamis Juma mwaka 1953 mpaka 1957 kulikuwa na chapisho la pili na baadae kuwa na chapisho la tatu mwaka 1958 mpaka 1966. Amesema kuwa katika mwaka 1967 mpaka mwaka 1972 machapisho ya makusanyiko ya uamuzi wa Mahakama Kuu yalitolewa (High Court Digests 1967 mpaka1972) na mwaka 1973 mpaka mwaka 1979 taarifa za juzuu zilitolewa (The Law Reports of Tanzania 1973-1979) kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mhe. Prof. Juma ameendelea kueleza kuwa baadae kuanzia mwaka 1980, Bodi ya Uhariri wa Juzuu ya Taarifa za Sheria ilibadilika na kuwa na uenyekiti kupitia Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Barnabas Samatta na kuanzia kipindi hicho Mahakama ya Tanzania iliendelea na shughuli za uchapaji wa machapisho yote.

Aidha Mhe. Jaji Mkuu ametoa pongezi na shukrani za dhati kwa Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa ufadhili kwa Mahakama ya Tanzania kwa kuwezesha na kufanikisha matoleohaya ya vitabu hivi vya kisheria kwa miaka yote hii na Faharisi za Sheria Mama na Sheria ndogo za kuanzia Mwaka 1961 mpaka 2020, vyote vikiwa katika mfumo wa nakala laini na nakala ngumu.

“hawa wamekuwa wadau wakubwa wa utoaji haki katika mashauri ya ngazi zote za Mahakama na wamekuwa wanasaidia Mahakama ya Tanzania katika mambo mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa utoaji haki,” amesema Jaji Mkuu.

Jaji Mkuu ameahidi kuwa Mahakama itaendelea kuimarisha upatikanaji wa nakala za maamuzi kwa miaka ya nyuma kuanzia mwaka 1980 mpaka Mwaka 2006. Aidha ameomba Mahakama kupitia Idara ya Menejimenti ya Mashauri na Kitengo cha Maktaba kuendeleza utaratibu huo wa kuandaa Faharisi ya Sheria Mama na Sheria ndogo kuanzia mwaka 2021 na kuendelea.

Naye , Jaji kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe, Mustapher Siyani ameeleza kuwa Juzuu za Taarifa yaa Sheria hizi ni nyenzo muhimu za kazi kwa kila mwanataaluma ya sheria nchini kwa kuwa kutokana na taarifa hizo maamuzi mbalimbali ya mashauri yanayoakisi msimamowa sheria katika nchi yetu yatapatikana.

Vilevile mesema kuwa taarifa hizo zitawasaidia wananchi na Mawakili wanaofika mahakamani kila siku kutafuta haki kujua misimamo mbalimbali ya kisheria kupitia uamuzi ya Mahakama za juu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Mratibu wa Bodi ya Uhariri wa Majuzuu ya Taarifa za Sheria Tanzania, Mhe Kifungo Mrisho amesema kuwa kabla ya kuwepo kwa machapisho hayo kumekuwepo na mchakato mrefu, ikiwemo kuingia katika Mahakama Mtandao na masuala ya TEHAMA ili kuwezesha kupata uamuzi wa mashauri mengi ya Mahakama Kuu Tanzania Bara na Visiwani sambamba na Mahakama ya Rufani, hatua ambayo imewezesha upatikanaji wa taarifa zote kuanzia mwaka 2007 mpaka 2020.

Uzinduzi wa Juzuu hizo umefanyika leo tarehe 24 Januari, 2022 katika Viwanja vya Nyerere Square vilivyopo katikati ya Jijini la Dodoma na kuhudhuriwa na watumishi pamoja na Viongozi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma.