Habari

Imewekwa: Sep, 22 2023

MHE. BALOZI DKT. PINDI HAZARA CHANA AIPONGEZA OFISI YA WAKILI MKUU WA SERIKALI

News Images

Tarehe 13 Septemba 2023, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb), amefanya ziara yake kwa mara ya kwanza ya kutembelea Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) iliyopo jijini Dar es Salaam tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongoza Wizara hiyo.

Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema kuwa lengo la ziara yake ya kutembelea OWMS ni kufahamu majukumu yao na kujenga uelewa kuhusu namna wanavyotekeleza majukumu hayo ili taasisi zote zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria ziweze kushirikiana kuhudumia wananchi kwa kuhakikisha nchi inazingatia misingi ya haki na utawala bora ili taifa la Tanzania liendelee kuwa taifa la amani.

Pia, ameipongeza OWMS kwa kulinda haki na maslahi ya Serikali yasipokonywe ndani na nje ya nchi kwa kushinda kesi ambazo Serikali ilikuwa na haki na kuwa mabingwa katika kutetea vyema Serikali.

“Vile mnavyoitetea Serikali na kushinda kwenye kesi zile ambazo Serikali ilikuwa na haki zile fedha ndiyo zinasaidia kuleta maendeleo ambapo tunajenga barabara, vituo vya afya, n.k. Ofisi hii ni muhimu ndiyo maana imekuwa Ofisi maalum. Ofisi hii ya Wakili wa Serikali kama vile tunavyofahamu wale Mawakili wengine wanalinda na kutetea maslahi iwe ni ya taasisi au ya mtu mmoja, sasa yeye ni Wakili Mkuu wa Serikali,” amesisitiza Balozi Dkt. Pindi Chana

Vile vile amesema kuwa ni muhimu kuwaeleza watanzania utaratibu wa Serikali wa kutoa notisi pale ambapo mtu anakuwa na jambo na Serikali anatakiwa atoe taarifa badala ya kufanya kienyeji bila kufuata utaratibu, “unatakiwa utoe notisi pale ambapo una jambo lako, maoni au kuuliza Serikali vinginevyo utakutana na mabingwa wa sheria watakukumbusha utaratibu,” amesisitiza Balozi Chana.

Ameielekeza OWMS kuwa tayari kupokea Ofisi zote za Serikali na kuwapa ushauri stahiki ili taratibu ziweze kuzingatiwa na Serikali isiingie kwenye hasara yeyote itakayosababisha upotevu wa fedha za Serikali. Amesisitiza Ofisi za Serikali zizingatie sheria, taratibu na miongozo hususani kwenye masuala yote ya madai na wapate ushauri ili kulinda maslahi ya Serikali na nchi kwa ujumla

Ameongeza kuwa milango ya Wizara ya Katiba na Sheria ipo wazi, hivyo taasisi za Serikali zinapokuwa na masuala wasisite kuwasiliana na Wizara, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na OWMS kwa kuwa kazi yetu ni kuwashauri, kuwasikiliza, kuwapa maoni na kuwakumbusha kuhusu utaratibu wa mashauri ili pale mtu anapokuwa na haki yake izingatiwe kwani sisi tumeapa kulinda haki za watanzania na taasisi.

Akitoa taarifa kwa niaba ya OWMS, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende amesema kuwa OWMS ina jukumu la kuendesha mashauri mbalimbali ya madai na usuluhishi ndani na nje ya nchi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake. Aliongezea kuwa OWMS pia inashiriki kuendesha mashauri yanayohusu Makampuni ambayo Serikali ina hisa, kwa mfano hivi karibu imeendesha shauri la benki ya CRDB lenye thamani ya shilingi bilioni 33.

Dkt. Luhende ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwake OWMS imeweza kumaliza mashauri mbalimbali kwa njia ya majadiliano, ikiwamo shauri lililohusu ujenzi wa SGR lililofunguliwa nchini Rwanda. Pia, OWMS imeendesha shauri lililofunguliwa Baraza la Usuluhishi la London ambapo Serikali ilikuwa inadaiwa shilingi trilioni saba na kufanikiwa kumaliza shauri hilo kwa majadiliano. Hivyo, kuwezesha Serikali kuepuka kulipa fedha hizo.

Amesema kuwa pamoja na OWMS kushinda katika kuendesha kesi na mashauri kwa majadiliano nje ya mahakama, OWMS imekuwa inakabiliana na changamoto mbali mbali kama vile baadhi ya taasisi za Serikali kuvunja mikataba au makubaliano ya kisheria waliyoingia na mtoa huduma au mkandarasi bila kuishirikisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hivyo kuzalisha migogoro inayokiuka sheria za mikataba, baadhi ya taasisi za Serikali zinachelewesha malipo ya huduma kwa wakandarasi hivyo kupelekea kufunguliwa kwa mashauri ya madai dhidi ya Serikali ambapo miradi hiyo ingesimamiwa vizuri ingeepuka milolongo ya kuiingiza Serikali katika madai na migogoro isiyoisha na baadhi ya taasisi kutokutoa au kutoa ushirikiano hafifu wakati wa kuandaa nyaraka mbalimbali zinazohitajika mahakamani na usimamizi hafifu wa miradi hasa miradi ya ujenzi ambayo imepelekea kuleta migogoro inayoenda kwenye suala la usuluhishi

Hali kadhalika, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana ameitaka OWMS na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria kuzikumbusha taasisi za Serikali, Ofisi za halmashauri, Wilaya, kata na vijiji vyote na watendaji wote nchi nzima kuzingatia utawala bora, misingi ya sheria na haki ili wananchi wanapokuwa na maswali au wanahitaji ufahamu kwenye masuala mbalimbali kama mirathi, ardhi na ushauri wa masuala ya madai wajibiwe kwa wakati. Mhe. Waziri Balozi Dkt. Pindi Chana amesisitiza kuwa Mhe. Rais Dkt. Samia ameweka Ofisi hizi kwa ajili ya watanzania hivyo ni muhimu kwa watanzania kufahamu haki zao na wasiwe wanyonge.