Habari

Imewekwa: Jan, 03 2022

Mahakama yaamuru Serikali kulipwa ada za uendeshaji wa Mashauri

News Images

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imesema kuwa Serikali inastahili kulipwa ada ya kuendesha Mashauri kama ilivyo kwa Mawakili binafsi huku ikisisitiza kuwa kupitia fedha hizo serikali inaweza kuanzisha mfuko maalumu wa uendeshaji wa Mashauri (Special Litigation Fund).

Kauli hiyo imetolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Yose Mlyambina wakati akisoma uamzi katika shauri la madai Na. 642 la mwaka 2020, lililohusu maombi ya madai ya gharama za uendeshaji wa Mashauri kwa upande wa Serikali.

Katika shauri hilo upande wa mlalamikaji ulidai kuwa Serikali haipaswi kulipwa gharama za maelekezo ya Mawakili wa Serikali kuendesha Mashauri ya Serikali kwa mwombaji kutoa hoja kuu tatu zilizodai kuwa, moja, Serikali hailipi ada yoyote Mahakamani, pili, Mawakili wa Serikali wanalipwa na Serikali kutokana na kodi ambayo hukusanywa kutoka kwa walipa kodi wakiwemo waombaji na Tatu, katika kuendesha Mashauri Mawakili wa Serikali wanatimiza wajibu kwa Umma.

Upande wa serikali ukiwakilishwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali walipinga vikali hoja hizo kwa kuwasilisha mahakani hapo hoja nne ambapo mawakili wa Serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu George Mandepo waliieleza Mahakama hiyo kuwa Serikali inapaswa kutunukiwa gharama sawa na Mawakili binafsi, lakin pia Mawakili binafsi hawana tofauti na Mawakili wa Serikali katika kutekeleza majukumu yao.

Akiwasilisha utetezi wake Mandepo alieleza kuwa Sheria ya Mawakili Sura ya 341, Juzuu la Marejeo ya Mwaka 2019, inasema Mawakili wa Serikali wanatambuliwa kama Mawakili na hivyo, Kanuni zinazosimamia malipo kwa Mawakili hazikumaanisha kuwatenga Mawakili wa Serikali wasilipwe gharama za maelekezo ya kuendesha Mashauri, hivyo ili kulipwa gharama za kuendesha Mashauri haihitajiki kuthibitisha gharama zilizotumika kwa kuleta stakabadhi za matumizi.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kuchambua Sheria na Mashauri mbalimbali Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam Mhe. Mlyambina alikubaliana na utetezi uliotolewa na upande wa Serikali kwa kusema kuwa Serikali inapaswa kulipwa gharama hizo kwa sababu mhusika aliyeshinda Shauri la Madai lazima arudishe gharama za Shauri kutoka kwa upande ambao haukufanikiwa, zaidi ya hayo, mhusika aliyefaulu hapaswi kunyimwa gharama isipokuwa kwa ''sababu nzuri' au sababu zinazokubalika au isipokuwa kuwe na mazingira maalum au mahsusi ya kufanya hivyo

Mhe, Mlyambina aliongeza kuwa Mawakili wa Serikali wanachukuliwa kuwa ni Mawakili kwa madhumuni ya utendaji wa kisheria kama Maafisa wa Mahakama. Hata hivyo, sheria ya sasa inayosimamia malipo ya Mawakili haitoi ada au malipo mahususi kwa Mawakili wa Serikali wanaoshughulikia Mashauri ya Serikali Mapungufu hayo yanahitaji kushughulikiwa katika sheria zetu hasa ukizingatia kuwa kwa mujibu wa Kifungu cha 30 (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Madai, Sura ya 33 Juzuu ya Marejeo ya 2019, utoaji wa gharama uko katika busara (discretion) ya Mahakama.

Aidha Mheshimiwa Jaji katika uamzi wake alibainisha kuwa hakuna ubishani kwamba Serikali haiwezi kushughulikia mgogoro au Shauri lolote katika Mahakama au Mabaraza ya Ushuluhishi pasipo kuingia gharama ambazo ni wazi zinatumika kutoka kwa fedha za umma na pia Mawakili wa Serikali wanapoendesha Mashauri kutoka Wizara, Idara au Taasisi za Umma kunajenga uhusiano wa Wakili na Mteja hivyo Katika hali hiyo, Ofisi ya Wakili Mkuu inashughulikia Shauri kama kampuni nyingine yoyote ya Uwakili na katika muktadha huo, Ofisi ya Wakili Mkuu ndiyo Wakili wa Umma hivyo inapaswa kulipwa ada za gharama ya uendeshaji wa Mashauri kama inavyofanyika kwa Mawakili binafsi.

Akitoa mfano, Mhe. Jaji alisema kuwa katika nchini nyingine kama vile India, ada na malipo ya Maafisa wa Sheria na Wanasheria wa Serikali kwa kushughulikia mashauri ya kisheria kwa niaba ya Serikali zimewekwa wazi katika Sheria, Utaratibu huo unaweza kutumika hapa nchini ili kusaidia Mahakama katika kuamua kwa urahisi stahili za malipo kwa Mawakili wa Serikali.

Mhe. Jaji alifafanua kuwa katika mashauri yanayohusu Serikali ipo haja ya Serikali kuweka mfumo wa Wizara na Idara za Serikali kuwa zinalipa ada ya Malekelezo kwa Wakili Mkuu wa Serikali kwa ajili ya kugharimia usimamizi na uendeshaji wa mashauri zinazoihusu Serikali. Ada hizo zinapodaiwa Mahakamani baada ya Serikali kushinda mashauri, ziwe zinarejeshwa moja kwa moja kwenye Ofisi inayohusika na uendeshaji ambayo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali au Wakili Mkuu wa Serikali kwa kadiri itakavyokuwa.

Katika hatua nyingineMahakama ilielekeza kuwa Serikali inaweza kuanzishwa Mfuko Maalum wa Mashauri (Special Litigation Fund - SLF) ambao chanzo chake kinaweza kujumuisha gharama zinazolipwa kwa Serikali kutoka kwenye Shauri za madai au usuluhishi ambazo Serikali imeshinda kwa kuwa gharama zinazolipwa kama fidia ni mapato ya umma kama ilivyo katika sekta nyingine za uzalishaji ambazo Serikali hupata mapato kwa njia ya kodi,ushuru, ada, ushuru au adhabu au tozo.

Mfuko huu unaweza kuanzishwa kisheria na sheria ikatoa masharti yanayosimamia utoaji rasmi maelekezo ya ugharimiaji wa kila Shauri kwa Wakili Mkuu wa Serikali. Mahakama iliona kuwa Mfuko huo Maalum unaweza kufanana na Mifuko mingine ya Kisheria iliyoanzishwa kwenye sekta mbalimbali za umma ikiwamo Mfuko wa Barabara ulioanzishwa kwa lengo la kusaidia uendelezaji wa na fedha yake inatozwa kutokana na matumizi ya barabara na ushuru wa mafuta, usafiri, leseni, tozo za uzito wa magari, faini ya ukiukwaji wa Sheria za Barabara.