Naibu Wakili Mkuu wa Serikali ametoa rai kwa watumishi wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali (OWMS) kuongeza usikivu wa masikio yao kwa wadau wanaowahudumia kwenye mikoa 18 ambapo Ofisi hiyo ipo inaendesha mashauri ya madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali na taasisi zake nchini nzima
Hayo yameelezwa na Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Alice Mtulo alipokuwa kwenye ziara yake mkoani Tanga kukagua utendaji kazi wa Ofisi hiyo ya uendeshaji mashauri, mazingira ya kazi, mahusiano ya Ofisi na wadau na namna inavyohudumia taasisi nyingine za Serikali katika kuendesha mashauri yao kwa niaba ya Serikali na wananchi kwa ujumla
Akiwa ziara mkoani Tanga, Bi. Mtulo alipata fursa ya kuonana na watendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga na kuzungumza na Kaimu Jaji Mfawidhi, Mhe. Messe Chaba, Mhe. Jaji Hapiness Ndesamburo na Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, ndugu Hudi M. Hudi ambapo aliwaarifu kuwa anashukuru kwa ushirikiano ambao Mahakama wanaipatia Ofisi ya Wakili Mkuuu wa Serikali mkoa wa Tanga katika uendeshaji wa mashauri na ameona ni vema kuonana nao ili kupata maoni ya utendaji kazi wa watumishi wa Ofisi hiyo kwenye Mahakama kwa kuwa Mahakama ni wadau wa karibu wa Ofisi hiyo
Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Chaba alisema kuwa OWMS mkoa wa Tanga inaipa Mahakama ushirikiano mzuri, watumishi wanafanya kazi zao kwa wakati ila aliiomba OWMS kuangalia utendaji kazi wa Idara za Sheria kwenye Halmashauri za Mkoa wa Tanga ili zisizalishe migogoro ya ardhi ili kupunguza idadi ya mashauri ya ardhi mahakamani na wingi wa kazi kwenye Ofisi ya OWMS ya uendeshaji wa mashauri hayo. Ametoa rai kwa Halmashauri waachane na uendeshaji wa mashauri ya madai mahakamani na wafanye usuluhishi ili kupunguza migogoro ya mashauri ya ardhi mahakamani kwa kuwa Mkoa wa Tanga mashauri mengi ni ya migogoro ya ardhi
Bi. Mtulo amewapongeza watumishi wa OWMS mkoa wa Tanga kwa utendaji kazi mzuri na mahusiano mazuri na wadau ikiwemo mahakama, halmashauri, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, taasisi nyingine za Serikali na wananchi wa ujumla.
“Tuongeze usikivu wa masikio yetu kwa wadau ili tuweze kuyashughulikia maoni ya wateja tunaowahudumia ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, taasisi za Serikali na wananchi kwa ujumla,” amesisitiza Bi. Mtulo.
Bi. Mtulo ameambatana na baadhi ya wajumbe wa menejimenti wa OWMS kwenye ziara hiyo ikiwemo Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, Bi. Asha Hayeshi, Mkurugenzi wa Mipango, Bi. Theresia Mpangala, Mkurugenzi Msaidizi wa Udhibiti Ubora, Bi. Mercy Kyamba, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi, Bi. Hellen Lubogo na Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA, ndugu Aziz Makuburi.
Maoni