Habari

Imewekwa: Oct, 04 2019

Msiwe kikwazo kwa watumishi walio chini yenu

News Images

Wajumbe wa MenejimentiOfisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, wameaswa kutokuwa kikwazo wa watumishi walio chini yao, hatua itakayosaidia watumishi hao kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

Wito huo umetolewa leo na Naibu Wakili Mkuu mpya wa Serikali Bwa. Gabriel Malata, alipokuwa akizungumza na wajumbe hao katika kikao cha menejiment kilichofanyika ndani ya ukumbi wa ofisi hiyo leo jijini Dar es salaam.

Akizungumza na wajumbe hao ambao ni wakuu wa idara na vitengo mbalimbali katika ofisi hiyo, Bwa. Malata amewasihi Viongozi hao kutimiza wajibu wao ili waweze kuleta tija kwa taifa.

“Naomba tusiendeshe ofisi hii kama tunaendesha kitu cha mtu binafsi, naomba uendeshaji wa ofisi hii uwe wezeshi ili kila mtu atumize majukumu yake kwa wakati,” alisema Bwa. Malata.

Katika kuhakikisha anawajengea uwezo mawakili wachanga, Bwa. Malata ameahidi kuwa ataanzisha mpango kabambe wa kuhakikisha anawaandalia mafunzo mawakili hatua itakayosaidia kuwaongezea ujuzi utakao wasaidia kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

Aidha, amewashauri mawakili wenye kesi mbalimbali Mahakamani kufanya maandakizi ya kutosha kabla hawajaenda mahakamani ili kuweza kuyajua mashauri yao vizuri ikiwa ni pamoja na kujua na kuelewa kuwasiliana na mahakama kwa lengo la kujua Mahakama inataka nini kwa wakati sahihi.

Ili kuhakikisha ofisi hiyo inafanya vizuri katika sekta ya sheria, Naibu Wakili Mkuu huyo ameshauri kuwa, ni muhimu kwa ofisi hiyo kuwa na vitabu na nyaraka za kutosha zitakazowasaidia mawakili wake katika kujiongezea maarifa kuhusiana na kada hiyo ya sheria.

Bwa. Malata pia amewasihi wajumbe hao kuwa waadilifu kwa kuzingatia nidhamu wawapo kazini, kwani kwa kufanya hivyo wataweza kuwa mahili katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Akizungumza mara baada ya kumtambulisha kwa wajumbe hao, Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Clement Mashamba amewataka kumpa ushirikiano Naibu wakili Mkuu mpya, kwani kwa kufanya hivyo itamsaidia kutekeleza majukum yake kwa ufanisi hatua itakayoisaidia ofisi hiyo kuzidi kufanya vizuri kwa manufaa ya taifa zima.

Bwa. Gabriel Malata anachukua nafasi ya aliyekuwa Naibu Wakili Mkuu Dkt. Ally Possi, ambaye ameteuliwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Naibu katibu Mkuu katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kabla ya uteuzi huo Bwa. Malata alikuwa Kamishina wa kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu.